Vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, vimeazimia kutohudhuria sherehe za kuapishwa kwa rais mteule Dkt. John Magufuli kwa lengo la kuonesha msimamo wao wa kupinga mchakato wa uchaguzi wa rais uliofanikisha ushindi wake.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti mwenza wa Ukawa ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuwa viongozi wote wa Ukawa na wabunge wateule wameazimia kususia ili kuonesha ulimwengu kuwa hawakubaliani na matokeo hayo kwa kuwa katiba ya nchi aliyoiita mbovu hairuhusu matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani baada ya Tume kumtangaza mshindi.

Mbowe aliwataka wafuasi wa Ukawa pia kususia sherehe hizo zilizopangwa kufanyika leo katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wageni mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi.

“Tunatoa wito kwa wananchi wote, Watanzania wote wapenda mabadiliko na wapenda haki wote kutohudhuria shughuli hiyo,” imeeleza taarifa hiyo.

“Tunataka nchi na dunia nzima kwa ujumla ijue wazi kuwa hatukubaliani na mchakato wa uchaguzi hasa matokeo ya urais ambayo kwa mujibu wa katiba yetu mbovu, mwenyekiti wa Tume akishatangaza hakuna mahali pa kuyapinga.”

Akieleza kuhusu mchakato wa ujumuishaji wa matokeo ya urais, Mbowe amesema kuwa baadhi ya matokeo yaliyokuwa yanatangazwa na Tume yalikuwa tofauti na matokeo halisi yaliyokuwa yamebandikwa vituoni.

Ali Kiba Agusa Kiwango Cha Chris Brown, Rihanna, Justin Bieber, Sean Paul
Ndoa Ya Siri Ya Wema Sepetu Yapata Maelezo Ya Mhusika