Uchaguzi wa kuwapata Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na Manispaa ya Temeke utalazimika kurudiwa baada ya serikali kutangaza Wilaya mpya sita zikiwemo wilaya mbili zinazozigawa Halmashauri hizo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene ameeleza hayo jana wakati akitoa taarifa kuhusu uamuzi wa Rais John Magufuli kuridhia kuanzishwa kwa mkoa wa Songwe pamoja na wilaya hizo.

“Kurudiwa kwa uchaguzi wa wa Kinondoni na Temeke hilo halikwepeki. Serikali inafanya haraka kuanzisha mamlaka na ukishakata utawala lazima uchaguzi utatakiwa kurudiwa, na hilo sio jambo geni,” alisema Waziri Simbachawene.

Alisema kuwa kwa kawaida wilaya hizo mpya zitatakiwa kuwa na viongozi ambao wamewachagua na kwamba madiwani watagawanyika kutoka katika halmashauri za mwanzo. Hivyo, watakata kuwa na viongozi waliowachagua.

Halmashauri hizo za zilishafanya uchaguzi ambapo Boniface Jacob (Chadema) alishinda nafasi ya Umeya wa Kinondoni huku Charles Kuyeko (CCM) akishinda Umeya wa Temeke.

Akizungumzia kurudiwa kwa uchaguzi huo, Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob alisema kuwa yeye atahamia katika Wilaya ya Ubungo.

“Nitakwenda kugombea Ubungo,” alisema Meya huyo wa Kinondoni.

“Hata hivyo, Kinondoni pia bado itabaki chini ya Ukawa kwa sababu tuna hazina ya kutosha ya madiwani pamoja na wabunge wa viti maalum,” aliongeza.

Naye katibu wa Chadema Kanda ya Dar es Salaam, Henry Kiwelo alieleza kuwa Ukawa hawana wasiwasi na mgawanyo pamoja na marudio ya chaguzi hizo kwa kuwa wanafahamu kuwa watashinda.

Kwa upande wa CCM, Katibu wa Uendezi wa chama hicho Tawala, Juma Simba alipotafutwa alieleza kuwa alikuwa kwenye kikao na asingeweza kuzungumzia suala hilo.

Chanzo: Mwananchi

Malale Hamsini Aendelea Kuzigonganisha JKU, Ndanda FC
Roger Federer Kupumzika Kwa Mwezi Mmoja