Juhudi za kutafuta muafaka wa kisiasa baada ya tangazo la kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu visiwani Zanzibar zinaendelea ambapo jana rais John Magufuli alikutana Ikulu ya Dar es Salaam na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad.

Kikao cha rais Magufuli na Maalim Seif kilihudhuriwa pia na Makamu wa rais Bi. Samia Suluhu Hassan ambapo wote walijadili hali ya kisiasa visiwani Zanzibar na muelekeo wa kupata muafaka.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, Maalim Seif na rais Magufuli walieleza kufurahishwa na hali ya amani na utulivu inayoendelea Zanzibar pamoja na muelekeo wa mazungumzo kati ya pande zote mbili.

“Rais Magufuli pia amewapongeza na kuwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kudumisha amani na utulivu, wakati mazungumzo baina ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), yakiendelea huko Zanzibar,” ilieleza taarifa hiyo ya Ikulu.

Iliongeza kuwa rais Magufuli alifurahishwa na taarifa ya Maalim Seif kuhusu mazungumzo yanayoendelea visiwani Zanzibar na kuisifia kuwa inaweza kuleta hali ya uelewano visiwani humo.

“Wote kwa pamoja wamewaomba wananchi waendelee kuwa watulivu ili kutoa nafasi ya majadiliano yanayoendelea kufikia hatma njema. Wameelezea matumaini yao kuwa vyama vya CCM na CUF haviwezi kushindwa kupata suluhu ya mgogoro huo,” ilieleza taarifa hiyo.

Hivi karibuni, Marekani kupitia Shirika la Changamoto la Milenia (MCC) ilisitisha mpango wa kuisaidia Tanzania zaidi ya shilingi trilioni 1 kutokana na kutoridhishwa na hali ya kisiasa nchini Zanzibar husan kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu waliouelezea kuwa ulikuwa huru na haki.

MCC walimtaka rais Magufuli kuingilia kati na kusaidia kufikia muafaka wa kisiasa nchini humo kwa kuzingatia utawala borana demokrasia.

Chadema wapaza sauti za Kilio Chao Kwa rais Magufuli
Waziri Kitwanga Ayakwepa Majina ya Wauza 'Unga'