Serikali mkoani Kagera imewaruhusu kurudi katika makazi yao ya awali wananchi 21 ambao walihamishwa kwa muda kutokana na Nyumba zao kuzingirwa na maji ya mvua kubwa iliyonyesha mei 26 mwaka huu na kusababisha mafuriko makubwa katika Manispaa ya Bukoba.

Akitoa taarifa ya awali ya tukio hilo mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jeneral Marco Gaguti amezitaja athari zilizojitokeza kuwa kifo cha mtoto mmoja mwenye umri wa miaka 10, Nyumba 1 kubomoka na nyingine 32 kuharibiwa.

Amesema kuwa wakazi 21 wa manispaa ya Bukoba waliokuwa wameondolewa kwenye makazi yao kwa sababu za kiusalama wameruhusiwa kurejea kwenye makazi yao baada ya maji kupungua katika maeneo yao na kuwataka kuchukua tahadhari kwa kipindi hiki mvua zinapoendelea kunyesha.

Aidha, amewataka kuchukua tahadhari kutokana na maji yanayoendelea kutiririka katika maeneo mbalimbali yakiwa yamechanganyikana na uchafu ili kuepuka magonjwa ya mlipuko.

“Mvua bado zipo watoto wadogo wadhibitiwe na wazazi pamoja na walezi hasa katika kipindi hiki cha mvua ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea,”amesema RC Gaguti.

Gaguti ameongeza kuwa licha ya mvua zinazoendelea kunyesha chanzo kikubwa cha mafuriko yaliyotokea ni uharibifu wa mazingira katika mkondo wa maji katika mto Kanoni.

Hata hivyo, amesema kuwa serikali ya Mkoa itachukua hatua za ziada kuhakikisha ujenzi holela unadhibitiwa, waliojenga bila kufuata taratibu wanaondolewa na kuongeza kuwa lazima sheria na taratibu za ujenzi zizingatiwe hasa maeneo tengefu ya mito.

Watendaji wa Serikali wilayani Longido washambuliwa
Watuhumiwa wa 'Tereza' watiwa mbaroni

Comments

comments