Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani limefanikiwa kuwanasa wezi wa gari la Afisa wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) wakijaribu kulitorosha usiku wa manane, ndani ya saa 12 tangu walipopata taarifa za tukio hilo la wizi.

Wezi hao wamedaiwa kuliiba gari la Afisa huyo wa JWTZ aliyetajwa kwa jina la innocent Dallu alilokuwa amelipaki katika eneo la Mbezi Juu jijini Dar es Salaam majira ya saa sita mchana, huku ndani yake kukiwa na watoto wake wawili lakini kabla ya kutokomea nalo walimshusha mtoto mmoja na kuondoka na mmoja.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonventura Mushongi alisema kuwa Jeshi hilo lilifanikiwa kuwanasa wezi wa gari hilo aina ya Toyota Harrier T400 DEH walipokuwa wakijaribu kulivusha katika eneo la Barabara ya Bagamoyo-Msata, kata ya Kiwangwa juzi majira ya saa 6 usiku.

Aliwataja waliokamatwa na gari hilo kuwa ni Ezekiel Daudi (25) ambaye ni mkazi wa Moshi aliyekuwa kwenye gari hilo huku Joshua Adam aliyekuwa analiendesha akitokomea vichakani baada ya kuwakabidhi polisi leseni yake ya udereva na kujifanya anakagua gari hilo kabla ya kutimua mbio.

“Joshua alitoroka baada ya kuwakabidhi leseni polisi, alijfanya naye anakagua gari lakini alitorokea vichakani. Joshua alikabidhi leseni yake ya udereva yenye namba 4001944688,” Kamanda Mushogi anakaririwa.

Akizungumzia jinsi walivyompata mtoto aliyekuwa kwenye gari hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Suzan Kaganda alisema kuwa walifanikiwa kumpata mtoto huyo majira ya saa 3:30 usiku akiwa ametelekezwa na mtu mmoja ambaye hakujulikana katika baa ya Golden Bridge iliyoko Kawe.

Alisema kuwa mhudumu wa bar hiyo ndiye aliyepelekea kupatikana kwake baada ya mtu aliyekuja naye kumuacha baani hapo akidai anaomba amuangalizie akatafute vibanda vya simu pesa, lakini hakurejea tangu saa 11: 30 jioni hadi usiku huo.

Askari huyo wa Jeshi alikuwa akifanya kazi katika hospitali ya Lugalo kabla ya kuhamishiwa Dafur, na alikuwa amerudi nchini kwa ajili ya mapumziko.

Picha: Majaliwa ahutubia kwenye kilele cha maadhimisho miaka 55 ya UDSM
Vigogo watatu bandari kortini kwa rushwa