Kitengo cha uhamiaji nchini Ghana kimesema kuwa waliobadilisha rangi ya miili yao maarufu kama kujichubua na wenye michirizi mwilini hawana vigezo vya kupata ajira.

Taarifa hiyo iliyotolewa na msemaji wa kitengo hicho imeeleza kuwa wote waliotuma maombi ya kazi wakati wa zoezi la kukusanya wafanyikazi wapya na wakawa na tatizo hilo wamewaondolewa sifa za kupata ajira kwa sababu wanaweza kupata majeraha na kutokwa na damu wakati wa mafunzo.

Taarifa hiyo imepingwa vikali na Waghana na kuiita ya kibaguzi huku baadhi wakikasirishwa zaidi na waliondolewa vigezo kwa sababu ya kuwa na michirizi mwilini, huku baadhi wakiisifia hatua hiyo ya kuwaondolea vigezo.

Mbali na michirizi na kujichubua, pia wenye michoro mwilini (tattoo) na wenye rasta hawata pata ajira nchini humo.

Wanaotuma maombi ya kutaka ajira wanapitia vipimo vya mwili na afya kama sehemu ya zoezi la kuwachuja wenye vigezo.

Takribani watu 84,000 wametuma maombi ya kazi hiyo, huku wanaohitajika wakiwa ni 500 pekee.

Hata hivyo, Mbunge mmoja, Richard Quashigah, amesema kuwa waombaji waliokataliwa wanaweza kuwapeleka waajiri hao mahakamani.

Chid Benz atiwa mbaroni kwa mara nyingine
Video: Zaidi ya Trilioni 7.87 zakusanywa na TRA kwa nusu mwaka