Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni (WHO), Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema watu hawapaswi kujisahau wala kuchukulia kama janga la Uviko-19 limeisha kwani bado lipo na linaendelea kuuwa mamilioni ya watu.

Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Geneva Uswisi, Dkt. Tedros amesema, “Hatuwezi kusema tunajifunza kuishi na Uviko-19 wakati watu milioni moja wamekufa kutokana na maradhi ya Uviko-19 kwa mwaka huu pekee.”

Amesema, kwa miaka miwili na nusu ya janga la Uviko-19 duniani kumekuwepo kuwa na nyenzo zote zinazohitaji za kuzuia vifo vitokanavyo na janga hilo la maradhi ya Uviko-19.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni (WHO), Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Aidha, Dkt. Tedros ametoa wito kwa Serikali zote ulimwenguni kuimarisha juhudi zao za kutoa chanjo kwa wahudumu wote wa afya, wazee, na wengine walio katika hatari kubwa zaidi, mbinu itakayosaidia kuweza kufikia utoaji wa chanjo ya Uviko-19 kwa asilimia 70 kwa watu wote.

Hata hivyo, amepongeza juhudi za kuendelea kutoa chanjo na kusema “inafurahisha kuona kwamba baadhi ya nchi zilizokuwa na viwango vya chini zaidi vya chanjo sasa zinainuka hasa barani Afrika.”

“Inafurahisha sana kuona kwamba utoaji chanjo unazingatia makundi yanayohitajika kupewa kipaumbele huku nchi nyingi zikipiga hatua ya kuvutia katika kutoa chanjo kwa asilimia 100 ya wafanyakazi wa afya na asilimia 100 ya wazee,” amefafanua Dkt. Tedros.

Young Africans: Dawa ya Azam FC inachemka
Kocha Katwila afunguka kuanza vibaya Ligi Kuu