Wizara ya Afya nchini Uganda, imewaonya wananchi wake waliopona ugonjwa wa Ebola kuepuka kushiriki tendo la ndoa kwa angalau siku 90, baada ya kuruhusiwa kuondoka hospitalini.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Virusi ya Uganda, Profesa Pontiano Kaleebu amesema kuwa ijapokuwa ugonjwa wa Ebola hauorodheshwi kama ugonjwa unaosambazwa kupitia kwa ngono, yapo matukio ambapo watafiti wamepata virusi hivyo katika majimaji yanayotoka sehemu za siri za mwanaume baada ya kupona.

Onyo hilo linasema kuwa ni mbinu ya kudhibiti msambao wa ugonjwa huo na iwapo watashindwa kujizuia kwa muda huo basi watumie kinga.

“Kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani, damu ya wagonjwa wa Ebola itapimwa katika maabara ili kuhakikisha kuwa virusi hivyo haviko mwilini mwao tena. Hata hivyo, watu ambao wamepona ugonjwa huo hawafai kushiriki ngono, na iwapo ni lazima basi watumie mipira,” Wizara ya Afya ilisema.

Tahiti nyingine zinasema kuwa Nchini Liberia kwa mfano, mwanamke aliambukizwa ugonjwa wa Ebola baada ya kushiriki tendo na mwanamume aliyekuwa amepona ugonjwa huo.

Nchini Uganda, kisa cha kwanza kiliripotiwa mwezi huu katika Wilaya ya Mubende na kufikia Septemba 27, 2022, watu 23 walikuwa wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo.

Nchini Tanzania Waziri wa Afya Ummy Mwalimu aliutangazia uma kuwa na tahadhari ya ugonjwa huo wa Ebola ambapo alisema tahadhari zaidi ziendelee katika maeneo ya mipakani na nchi zinazotajwa kuripoti visa vya wagonjwa kadhaa.

Kocha Baraza afunguka alivyomsaidia Novatus Dismas
Putin kutangaza milki sehemu ya ardhi ya Ukraine