Jeshi la polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa udanganyifu kupitia mtandao wa kijamii wa facebook baada ya kufungua akaunti kwa kutumia jina la mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli.

Wanaoshikiliwa kwa tuhuma hiyo ni Sophia Mwaluanda (22), mfanyabiashara mkazi wa sisitila jijini Mbeya na Mpaji Mwinyimvua (38), mkazi wa Manzese, jijini Dar es salaam.

Taarifa iliyotolewa jana na kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Ulrich Matei imeeleza kuwa, watuhumiwa hao walikamatwa April 28, mwaka huu majira ya saa 9:00 alasiri katika msako uliofanyika maeneo ya Ikuti sokoni, tarafa ya Iyunga jijini Mbeya.

Amesema mbinu iliyokuwa ikitumiwa na watuhumiwa ni kufungua akauti facebook yanye jina la Janeth Magufuli Saccos na kuaminisha umma na kuweka picha yake na kisha kutangaza kutoa mikopo nafuu kwa sharti la muombaji kutuma kwanza fedha sh. 76,500 kwa namba ya simu waliyoweka kama ada ya mkopo kwaajili ya kupewa mkopo wa sh. 3,000,000.

Ameeleza kuwa watuhumiwa hao walikutwa wakiwa na simu mbili, moja simu janja ambayo ilitumika kufungua akaunti ya facebook na nyingine aina ya Scoo Mobile ambayo ilitumika kupokea fedha zinazotumwa na watu mbalimbali.

Kamanda Mtei amebainisha kuwa watuhumiwa hao walikutwa na fedha taslimu sh. 470, 000, walizokiri kuzipata kwa njia ya udanganyifu kupitia akaunti hiyo feki zilizotumwa na watu waliotaka kupata mkopo.

Aidha ametahadharisha kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao wawili ni mwendelezo wa operesheni inayoendelea kufanywa na polisi ili kuwapata watu wanaotumia majina ya watu maarufu wakiwamo viongozi na wasanii kufungua akaunti kwenye mitandao ya kijamii kwa ajili ya kujipatia fedha kwa udanganyifu.

Majaribio yaanza tiketi kwa mtandao nchi nzima
Parimatch yaja kibabe na mfumo mpya