Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) walioondolewa chuoni hapo siku kadhaa zilizopita kutokana na sababu mbalimbali zilizoainishwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kutokuwa na sifa za kusoma Stashahada maalum ya masomo ya Sayansi na Hisabati, wamejitokeza na kujitetea.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Gibson Jonson ambaye alijitambusha kama mwakilishi wa wanafunzi hao ameiomba Serikali kutumia busara kuwafikiria kuhusu suala lao kwani sio kweli kuwa wao ni vilaza (wanafunzi walishindwa katika masomo), bali walikwua na vigezo vya kujiunga na masomo hayo na hata kuendelea na kidato cha sita.

“Siyo kweli kwamba sisi ni vilaza na waliofeli na kupata daraja sifuri,” alisema.

“Sisi ni wanafunzi tuliofaulu kwa viwango vilivyohitajika kwa daraja la kwanza hadi la tatu na tulipangiwa shule za kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita, lakini tulibadili na kuamua kujiunga Udom, hivyo tunaomba Serikali itumie busara zake,” aliongeza.

Alisema kuwa hivi sasa hawawezi kujiunga tena na kidato cha tano kwakuwa tayari wameshapoteza muda chuoni hapo. Walimuomba Rais Magufuli pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Profesa Joyce Ndalichako kuwarudisha chuoni hapo ili wamalizie masomo yao.

Hivi karibuni, Serikali iliwaondoa UDOM wanafunzi zaidi ya 7000 ambao walikuwa wakisoma stashahada maalum ya Sayansi na Hisabati. Sababu mbili zilitolewa na Serikali kwa wakati tofauti ni pamoja na mgomo wa walimu waliokuwa wakiwafundisha wanafunzi hao waliokuwa wakidai fedha ambazo mkaguzi wa ndani aliainisha kuwa hazikuwa halali kiutaratibu wamalipo.

Pia, sababu kuu iliyoainishwa na Rais Magufuli ni kuwepo kwa wanafunzi wasio na vigezo vya kujiunga na masomo hayo katika ngazi ya Chuo Kikuu.

Rais Magufuli alisema kuwa Serikali itawatayarishia mazingira ya kuendelea na masomo yao wale watakaobainika kuwa na sifa lakini wasio kuwa na sifa wakatafute vyuo vinavyoendana na alama walizopata katika kidato cha nne.

Rais Magufuli atembelea kanisa la Mzee wa Upako, amuahidi haya
Mafarao Wazima Ndoto Za Taifa Stars Fainali Za Afrika 2017