Baada ya Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji kuwavua uanachama baadhi ya wajumbe wa klabu hiyo kwa idini ya wanachama waliohudhuria katika mkutano mkuu wa dharura, viongozi walivuliwa uanachama wamepeleka barua ya kupinga uamuzi huo katika Shirikisho la soka nchini TFF.

Msemaji wa TFF, Alfred Lucas amethibitisha kupokelewa kwa malalamiko ya viongozi hao wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam ambapo amesema barua hiyo iliwasilishwa katika shirikisho hilo Agosti 12, 2016.

“Kuna wanachama wakiokuwa viongozi wa Yanga waliotimuliwa uanachama Agosti 6, mwaka huu walileta barua ya malalamiko TFF, ” amesema Lucas.

Ameongeza kuwa “nathibitisha kuwa malalamiko yao yamepokelewa ambayo yanalenga kutaka haki itendeke.”

Amesema barua hiyo inasema kuwa uongozi wa Yanga ulikiuka taratibu na katiba ya klabu hiyo ilipowafuta uanachama.

“TFF imeyapokea malalamiko hayo na yatapelekwa katika kamati husika pindi yatakapofanyiwa maamuzi tutawajulisha wadau wa mpira wa miguu nchini,” amesema.

Wanachama waliovuliwa uanachama ni pamoja na Ayubu Nyenzi na Hashim Abdallah.

Harmonize afyatuka, ataka kuvaa ‘dera’ ili asifananishwe na Diamond
Mchungaji amuua Muumini wake akijaribu kuonesha muujiza