Rais  wa Shirikisho la soka nchini TFF Wallace Karia leo ameiaga timu ya vijana ya Kituo cha Watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Tanzania Street Academy (TSC) cha jijini Mwanza, itakayoshirikisho michuano ya Kombe la dunia kwa Watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu itakayofanyika nchini Urusi.

Timu hiyo imeondoka leo kwa ndege ya Shirika la Ndege la Qatar ikiwa na wachezaji 9 na viongozi 4 na kutimiza jumla ya watu 13 kwenye msafara wao.

Rais wa TFF Karia ameitakia kila heri timu hiyo katika safari yao, huku akiwataka wachezaji kufahamu wanabeba bendera ya Tanzania ambayo ina heshima kubwa, hivyo wahakikishe wanakwenda kufanya vizuri.

Amesema TFF inaamini timu hiyo itafanya vizuri kama ilivyokuwa mwaka 2014 waliporudi na kombe kutoka nchini Brazil kwenye mashindano kama hayo.

Naye Rais wa Taasisi hiyo ya TSC Altaf Mansoor ambaye pia ni mkurugenzi wa kampuni ya Moil ameshukuru ushirikiano mkubwa kutoka kwa TFF ambao wametekeleza kila kilichoombwa pamoja na serikali na sehemu iliyobaki ni kwa vijana hao kwenda kufanya vizuri na kurudi na kikombe.

Katika hatua nyingine Rais wa TFF Ndugu Karia amesema ili kuhakikisha TFF inajikita katika maendeleo ya mpira wa miguu TFF imewaachia Bodi ya Ligi kuwa huru kusimamia Ligi Kuu na Daraja la Kwanza na TFF inaingia pale tu wanapoona mambo hayaendi sawa.

Amesema TFF inasimamia zaidi sera,timu za Taifa na Ligi za chini ikiwemo Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) inayoendelea kwenye vituo vinne vya Geita,Rukwa,Singida na Kilimanjaro.

“Uongozi wangu umepunguza mzigo na kuacha huru vitu vingine vifanywe na Bodi ya Ligi kwa kuwaacha huru na sisi tunasimamia sera na timu za Taifa na mafanikio mnayaona na yatakuja mengi zaidi” amesema Karia.

Ameongeza kuwa ni vizuri watu kuwa na mtazamo chanya kuondokana na mtazamo hasi ambao siku zote hukimbiza wadhamini wanaotaka kuingia kwenye mpira wa miguu akiwataka wadau kubadilika katika mtazamo wao kwakuwa hata TFF iliyopo madarakani tayari imebadilika.

Kiongozi wa matawi Young Africans aishutumu TFF
Zilizopanda daraja 2018/19 zatangazwa rasmi