Katibu mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa na Mtendaji wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura leo wametoa ushahidi mahakamani kwa upande wa Jamhuri juu ya kesi inayowakabili maafisa wa shirikisho hilo ya kujihusisha na rushwa ili wapange matokeo.

Katika kesi hiyo inayosikilizwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, washitakiwa Martin Chacha na Juma Matandika ambao walikuwa maafisa wa TFF wanashitakiwa kwa kuomba rushwa toka kwa uongozi wa timu ya Geita Gold Mining ili wapange matokeo.

Washitakiwa hao, katika ushahidi uliorekodiwa wanasikika wakidaiwa kuomba rushwa ya Sh milioni 25 ili waisaidie timu hiyo kupanda daraja.

Wakiongozwa na Wakili wa Serikali Leonard Swai wamesema ilikuwa ni rahisi kwao kuzitambua sauti za watuhumiwa hao ambazo zilikuwa zimesambazwa katika vyombo mbalimbali vya habari pamoja na mitandao ya kijamii kwani walikuwa wakifanya kazi na watuhumiwa kwa muda mrefu.

Wamesema kutokana na uzoefu waliokuwa nao katika kufanya kazi nao kwa Zaidi ya miaka miwili iliweza kuwafanya wao watambue sauti za maafisa hao pindi walipoweza kusikiliza katika redio pamoja na Taasisi ya kupambana na Rushwa(PCCB).

Akitoa maelezo yake mbele ya hakimu Shahidi, Mwesigwa alidai kuwa anaamini sauti iliyorekodiwa ni ya maofisa hao kutokana na sauti pamoja na mambo yaliyokuwa yakizungumzwa yalikuwa yakiwahusu viongozi hao.

Mwesigwa ameongeza kuwa  kwa upande wake Juma Matandika alijiuzuru katika nafasi yake aliyokuwa akiitumikia ya Kaimu Mkurugenzi wa mashindano TFF kutokana na kile alichodai nafasi hiyo ya kazi kutompa nafasi ya kuweza kufanya mambo yake binafsi mbali nay ale aliyokuwa akiyafanya yanayohusu soka la Tanzania.

Katika sakata hilo la kupanga matokeo timu mbalimbali ziliweza kushushwa daraja ikiwemo Geita Gold Mining, Morogoro JKT, Kanembwa JKT pamoja na Polisi Tabora.

Mbali na kushushwa daraja kwa timu hizo Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za wachezaji iliweza kuwachukulia hatua mbalimbali viongozi waliokuwa wakihusika na suala hilo ikiwemo kuwafungia kutojihusisha na michezo katika kipindi chote cha maisha na wengine walifungiwa kwa vipindi vya miaka kadhaa.

Hata hivyo kesi hiyo imehairishwa hadi january 24 mwakani ambapo mashaidi wengine watatu watatakiwa kufika mahakamani hapo ili kutoa ushahidi juu ya kesi hiyo .

TFF Kuratibu Tiba Ya Moyo Kwa Wachezaji
Rais Magufuli afanya uteuzi mwingine Ikulu