Wamiliki wa kampuni ya Jamii Media inayomiliki mtandao wa Jamii Forum jana walifungua shauri Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kupinga vipengele vya sheria ya makosa ya mtandao wanavyodai vinakinzana na katiba ya nchi kwa kubana uhuru wa ‘faragha’ na kutoa maoni.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Maxence Melo alisema kuwa vipengele vinavyomtaka mmiliki wa mtandao kuwasilisha polisi taarifa za mteja wake ambaye ametoa maoni fulani ni kinyume cha Ibara ya 18 ya Katiba ya nchi na inabana fursa ya wananchi kufichua maovu.

Alisema kuwa mtandao wa Jamii Forum utaendelea kuwapa nafasi wananchi kutoa maoni yao kwa maslahi ya taifa.

“Tuangalie suala lenyewe, je lina maslahi ya nchi… lina uongo?” Alihoji. “Sasa inashangaza, mtu anasema kwamba kuna Tembo wanauawa, unaenda kumtafuta yule aliyesema Tembo wanauawa kwanza umdhibiti yeye, badala ya kwenda kuwadhibiti wanaoua Tembo.

“Inatia shaka nia na lengo la wale wanaotaka kujua taarifa za watu binafsi wanaotoa taarifa kwa ajili ya kusaidia nchi yao,” aliongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media.

Nae wanasheria wake Benedict Alex, walieleza kuwa kutoa maoni na taarifa binafsi au faragha ni haki ya kikatiba ya kila mwananchi, hivyo kutaka taarifa za kila mtoa taarifa ziwekwe wazi kwa Jeshi la Polisi linakinzana na katiba.

Mtandao wa Jamii Forum ulipata umaarufu mkubwa na umekuwa ukitumika kama chanzo cha kutoa taarifa mbalimbali zinazotoa matokeo makubwa katika jamii, lakini wakati mwingine baadhi ya taarifa hizo huthibika kuwa sio za kweli.

 

Nyundo ya TRA kwa Profesa Tibaijuka kuhusu fedha za Escrow yafika ukingoni
Madiwani Ukawa wavamia ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji Dar