Klabu ya Simba kesho itafanya Semina ya Wanachama wote wa klabu hiyo kwa ajili ya kuwapa elimu ya mabadiliko.

Taarifa iliyotolewa na mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara inaeleza kuwa, semina hiyo inalenga kujenga uelewa mpana zaidi juu ya muundo mpya wa uendeshwaji wa klabu hiyo.

Hatua hiyo inafuatia mabadiliko ya Katiba ya Simba yaliyofanywa na wanachama wa klabu hiyo na kusajiliwa na Msajili wa Vyama vya Michezo na Klabu nchini.

“Maandalizi yote ya Semina hiyo yamekamilika,na itafanyika kesho tarehe 16 mwezi wa 8 mwaka 2017, ambayo itakuwa ni Jumatano kuanzia Saa Nane na Nusu mchana (8.30)”.

Semina hiyo itafanyikia kwenye ukumbi wa Mikumi uliopo kwenye eneo la maonyesho ya kimataifa ya biashara ya Sabasaba (PTA), Kurasini mjini Dar es Salaam.

“Tunawaomba wanachama wote popote walipo waje kwa wingi hapo kesho, huku klabu ikiwaomba viongozi wa Simba Wilaya ya Temeke waandae utaratibu mzuri wa kuwapokea wageni,” Imeongeza taarifa ya Manara.

Uchaguzi Kamati Ya Uongozi TPLB
Mabosi wa klabu za England kuwasilisha mapendekezo FA