Wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) leo wamegoma wakipinga mabadiliko ya kiwango cha mkopo na utaratibu wa mgawanyo wa mkopo huo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza.

Makamu wa rais wa Serikali ya wanafunzi wa chuo hicho, Shamira Mshengema amesema kuwa wamechukua uamuzi huo kupinga punguzo kubwa la fedha za kujikimu kwa baadhi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza. Alisema awali wanafunzi wote wenye sifa ya kupata mikopo walikuwa wakilipwa kiasi cha shilingi 510,000 kwa miezi miwili (8,500 kwa siku) lakini sasa baadhi wanalipwa shilingi 19,000 tu kwa miezi miwili.

Mshengema amesema kuwa wamewataka wanafunzi hao kutosaini kiasi hicho cha fedha kwani haiwezekani mwanafunzi akaishi kwa shilingi 19,000 kwa miezi miwili.

“Kwakweli hali ni mbaya sana. Wanafunzi walikuwa wakipewa shilingi 510,000 lakini leo wanalipwa shilingi 19,000. Ina maana hata kwa wasichana wanawatengenezea mazingira magumu. Mwisho wa siku watu watashindwa kufuata masomo watajikuta wanaenda kufanya kazi tofauti,” Mshengema aliwaambia waandishi wa habari.

Naye Naibu Waziri wa Mikopo katika Serikali ya wanafunzi wa chuo hicho, Abdul Nondo alisema kuwa wanahitaji kukutana na Waziri ili wamueleze hali ilivyo mbaya kwa wanafunzi na kwamba hawatapokea kiasi hicho kidogo.

“Maisha ni magumu sana. Wengine hapa sisi wazazi wetu tukifika hapa kila kitu ni sisi wenyewe. Fedha ya kula na malazi ni wewe mwenyewe, hao mawaziri wote unaowaona leo, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya… walisoma kupitia mkopo uliokuwa ukitolewa,” alisema.

Wanafunzi hao pia walipinga utaratibu wa kutoa fedha za kujikimu kwa kuzingatia asilimia ya mkopo wa mwanafunzi husika, tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo katika fedha za kujikimu wanafunzi wote walipata kiwango sawa bila kujali asilimia za mkopo wa karo.

Jitihada za kumpata Katibu Mkuu au msemaji wa wizara hiyo ziligonga mwamba baada ya afisa aliyekuwa katika wizara hiyo kudai kuwa hawakuwa ofisini na kwamba waandishi walipaswa kuomba nafasi ili wizara ijiandae kuwapa majibu stahiki kwa kina.

Taarifa zilizoifikia Dar24 hivi punde, uongozi wa Jumuiya ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini wamekutana na uongozi wa wizara ya elimu. Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Stanslaus Abdugazile amesema kuwa wameafikiana kuwa Wizara itapitia tena utaratibu huo ili kuondoa changamoto zilizoibuliwa.

 

 

Serikali Yapunguza deni la mfuko wa hifadhi ya jamii
Mavugo Arejeshwa Kikosi Cha Kwanza