Sura ya Migomo ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) imeanza kurejea baada ya leo kufanyika mgomo uliotokana na kucheleweshewa fedha za kujikimu zinazotolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini (HESLB).

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi chuoni hapo, Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi, Shamila Mshengema alisema kuwa wameamua kufanya mgomo huo kutokana na kuwepo kwa majibu yasiyoeleweka kuhusu utolewaji wa mkopo huo.

Kwa mujibu wa taratibu, mkopo wa kujikimu kwa wanafunzi wa elimu ya juu hutolewa kila baada ya siku 60, lakini ratiba hiyo imekuwa ngumu kufuatwa na Bodi hiyo kutokana na sababu mbalimbali ambazo hata hivyo hushindwa kuwa za kuridhisha kwa wanafunzi.

Dar24 imeelezwa na baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Dar es Salaam Institute of Technology (DIT) wenye sifa za kupata mkopo kuwa kama ilivyo kwa wenzao wa UDSM, wamekubwa na tatizo la kucheleweshewa mikopo katika kipindi cha hivi karibuni.

Katika moja kati ya ahadi zake kwa wanafunzi wakati wa kampeni, Rais John Magufuli alisisitiza kuwa atahakikisha fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu zinatolewa kwa wakati.

Alisema kuwa anashangazwa na tabia ya Bodi ya Mikopo kuchelewesha fedha hizo wakati ni mkopo ambao wanafunzi wataurejesha.

Wauaji wa Albino washughulikiwe sasa.....
TEHAMA yarahisisha mfumo wa uombaji Ajira.