Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kagera inawashikilia wanafunzi wawili wa vyuo vikuu vya Dar es salaam na Mwenge wanaodaiwa kunufaika na Bodi ya Mikopo huku wakiwa ni raia wa Rwanda.
 
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Kagera, Pendo Buteng’e ambapo amesema kuwa pamoja na wanafunzi hao pia Watanzania watatu wanashikiliwa kwa madai ya kuwasaidia kutoa taarifa za udanganyifu.
 
Amewataja wanafunzi hao kuwa ni pamoja na Tumaini Francis anayesoma Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) na Peace Francis (Mwenge) wote wakiwa mwaka wa pili wa masomo, ni ndugu waliozaliwa hapa nchini huku wazazi wao wakiwa na uraia wa Rwanda.
 
Aidha, baada ya uchunguzi amesema kuwa Idara hiyo imebaini kuwa, Marie Msabima ambaye ni mama yao ni mfanyakazi katika kituo cha Bethania Christian Aid Foundation cha Kemondo Wilaya ya Bukoba akiishi kwa kibali mpaka mwaka 2020.
 
Mwenyekiti wa Kijiji cha Rwagati Kata ya Kemondo kilipo kituo hicho, Joseph Kinyonyi anashikiliwa na polisi kwa madai ya kusaini nyaraka kuthibitisha kuwa wanafunzi hao ni Watanzania wenye sifa ya kupata mkopo kutoka Bodi ya Mikopo.
 
Hata hivyo, kuhusu madai ya kusaini nyaraka za mikopo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Rwagati, Joseph Kinyonyi amesema kuwa alijua ni kama walivyo watoto wengine wanaolelewa katika kituo hicho ambao huchukuliwa mitaani na kupata msaada.
 

Wafungwa wamiliki simu Gerezani
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Machi 23, 2019