Wanafunzi nane waliomaliza kufanya mitihani yao ya kuhitimu elimu ya Sekondari nchini Kenya wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kufanya udanganyifu kwenye mitihani hiyo pamoja na kutoa lugha chafu dhidi ya Serikali.

Watuhumiwa hao walikamatwa kufuatia video iliyowekwa mtandaoni ikiwaonesha wakiwa wanasherehekea, wakidai kuwa wamefanya udanganyifu kwenye mitihani hiyo lakini hawatakamatwa.

Wanafunzi hao walienda mbali na kumtolea lugha za kejeli waziri wa mambo ndani pamoja na waziri wa elimu, kitendo kilichowaongezea kitanzi cha mkono wa sheria.

Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la polisi, wanafunzi hao nane walikuwa rumande kwa kipindi cha wiki moja wakati upelelezi wa kesi hiyo dhidi yao ukiendelea.

Mwezi uliopita, Serikali ya Kenya ilieleza kuwa imechukua hatua kali za kudhibiti udanganyifu katika mitihani, kitendo ambacho kimekuwa tatizo kubwa nchini humo.

Rais Uhuru Kenyatta alifanya ziara za kushtukiza katika baadhi ya shule za sekondari wakati mitihani ikiendelea, kwa lengo la kujionea namna ambavyo mitihani hiyo inafanyika. Baadhi ya wanafunzi, walimu na wasimamizi walikamatwa kwa tuhuma za kushiriki vitendo vilivyoashiria udanganyifu, ikiwa ni pamoja na wanafunzi kukutwa na simu kwenye chumba cha mitihani.

Bruno Genesio aihofia Manchester City
JPM amng'ata sikio Lowassa kuhusu Wapinzani