Serikali ya Tanzania, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Samia Suluhu Hassan imetoa matumaini ya kuimarika kwa mazingira ya uhuru wa vyombo vya Habari na kujieleza, licha ya uwepo wa baadhi ya vufungu vya sheria vinavyohitaji kufanyiwa marekebisho za vyombo na huduma za habari, zilizo na changamoto.

Hali hiyo, inatokana na kuchukuliwa kwa hatua kadhaa na Serikali, ikiwemo kufunguliwa kwa vyombo vya Habari vilivyofungiwa na kuanzisha mchakato shirikishi wa marekebisho ya sheria zinazoratibu tasnia ya habari.

Awali, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alikutana na makundi mbalimbali ya wanahabari wakiwemo wale walio chini ya mwamvuli wa Muungano wa Watetezi wa Haki ya kupata Taarifa (CORI).

Akizungumza na waandishi wa Habari mmoja wa Wanasheria maarufu nchini ambaye hakutaka kuandikwa kwa jina lake amesema, ipo haja ya kuweka sheria zitakazoendana na mazingira ya usasa.

“Dunia imebadilika, japo kila tawala zina zama zake na ni lazima kuwa na mipaka ya aina ya vitu vya kuripoti lakini hii haizuii kufanya marekebisho ya sheria rafiki kwa wanahabari na wamiliki wa vyombo vya Hbari nchini,” amesema.

Mchakato wa marekebisho ya sheria, unahusisha uwakilishi wa Wanahabari, wadau na Serikali ambapo kwa pamoja watazipitia sheria husika, kujadiliana na kufanya marekebisho muhimu yatakayojenga mazingira wezeshi ya uwepo wa uhuru wa vyombo vya habari, kujieleza na kupata taarifa.

Katika kufanikisha jambo hilo wakati wa mkutano Waziri Nape alielekeza kuundwa kwa timu ya Wanahabari itakayofanya majadiliano na timu ya Serikali, ili kupata sheria nzuri itakayostawisha muhimili huo muhimu nchini.

Hata hivyo, bado kuna changamoto ya ushiriki wa wanahabari wengi kutoshiriki ipasavyo katika mchakato huu, huku taasisi za MISA Tanzania na Baraza la Habari Tanzania (MCT), zikIwa mstari wa mbele kufuatilia na kuripoti ukiukwaji wa haki ya uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari.

Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Uhalifu wa Kimtandao ya mwaka 2015 ni miongoni mwa zinazopigiwa kelele na wadau wa habari kuwa chanzo cha wanahabari kukamatwa na/au kuwekwa vizuizini, vyombo vya habari kutozwa faini, na/au kufungiwa sambamba na ile ya kutaka usajili wa Gazeti kwa kila mwaka badala ya usajili wa kudumu.

Milioni 200 zaboresha miundombinu Hospitali ya Bombo
UN yataka uchunguzi vifo 23 vya Waafrika