Waandishi wa Habari wa Nyanda za Juu Kusini wamepewa mbinu za kukabiliana na majanga wawapo maeneo yao ya kazi ili kuweza kutekeleza majukumu yao kwa lengo la kuboresha na kuwaongezea uwezo wa kujiamini.

Mafunzo hayo ya siku tatu yametolewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) ambapo muwezeshaji mwanasheria, Deo Bwire amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwafahamisha kuhusiana na mazingira ya kazi.

‘’Kwasababu tunajua kazi ya wanahabari na mazingira yake ambayo kidogo yanakuwa hatarishi kipindi fulani, kwa hiyo hapa tunawapa mbinu mbalimbali za kuweza kujikinga na mazingira hatarishi ya kazi,”amesema Bwire

Amesema kuwa pia wanawafundisha waandishi namna ya kujua sheria za nchi na masuala mazima ya namna ya kuripoti habari ili wakiwa wanafanya kazi zao wasiende kinyume cha sheria.

Kwa upande wa mwanasheria, Jones Sendodo amesema kuwa kwa kushirikiana na Baraza la Habari MCT wamekuwa wakiwasaidia waandishi wa habari ambao wamekuwa wakipata majanga pamoja na kusimamia kesi zao mahakamani.

”Waandishi wa habari waendelee kutoa habari matukio yanayotokea kwenye jamii zetu kwa sababu tunaamini haki ya kupata habari ndio haki ya kwanza tusipohabarishwa hatuwezi tukajua, hatuwezi tukachukua hatua kwa hiyo naendelea kuwasihi waandishi wa habari muweze kuripoti matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu ili mwisho wa siku mamlaka na watu husika waweze kuchukua hatua  stahiki’’amesema Sendodo.

Rais wa Uturuki asimamia ndoa ya Ozil
Kila siku watu milioni moja huambukizwa magonjwa ya zinaa

Comments

comments