Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma linawashikilia wanajeshi nane wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa tuhuma za mauaji ya kijana mmoja na kumjeruhi mwanafunzi wa kidato cha kwanza mkoani humo.

Wanajeshi hao wanadaiwa kumpiga hadi kumuua, Erick Nilamewa mwenye umri wa miaka 16, waliyemtuhumu kwa kuwaibia simu aina ya Tecno na fedha kiasi cha shilingi 6,000.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Ferdinard Mtui, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi jioni mtaa wa Matatini Mwanga Manispaa ya Kigoma Mjini/Ujiji na kwamba jeshi hilo linaendelea kuwahoji na baadae litawafikisha mahakamani.

“Tunawashikilia wanajeshi nane na tunaendelea na upelelezi, na baada ya uchunguzi tutawapeleka mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake,” alisema Kamanda Mtui.

Naye majeruhi wa tukio hilo, Mussa ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya Sekondari ya Kitwe alieleza kuwa alipigiwa simu na wanajeshi hao waliomweleza kuwa wanamhitaji.

 

Alisema kuwa aliitikia wito wao kwakuwa anawafahamu na huwa anaingia katika makazi yao lakini alipofika aliambulia kipigo kikali akitakiwa kuonesha alipoficha simu na fedha zao.

“Waliniambia ninyooshe miguu yangu juu ya ukuta na niliponyoosha walinipiga na ubao na fimbo ya mianzi kichwani… damu zilianza kutoka. Wakachukua maji wakasafisha, wakapiga tena kichwa nikaanguka chini kisha wakanipiga mateke na kunichapa na nyaya za umeme huku wakiuliza ilipo simu na Sh 6,000 nilizoiba,” Mussa alisimulia akiwa kitandani, hospitalini.

Mbunge Afunguka walivyoitiwa 'Rushwa' kwa lugha tamu
Lil Kim atangaza rasmi ujio wake mpya