Takribani watu 10 wameripotiwa kuuawa kwa kukatwa vichwa Kaskazini mwa Msumbiji na watu wanaosadikika kuwa magaidi wa kundi la Al-Shabaab la eneo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na vyombo vya usalama nchini humo, watoto na wanawake ni kati ya waliouawa kikatili katika kijiji cha Monjane katika eneo la Cabo Delgado ambalo ni maarufu kwa uchimbaji wa madini na nishati ya mafuta.

Wapiganaji wa kundi hilo la kigaidi lenye itikadi kali ya kidini limekuwa likifanya mashambulizi ya mauaji ya kikatili katika mkoa huo mwaka jana.

Mmoja kati ya wakaazi wa kijiji cha Monjane aliliambia shirika la habari la AFP kuwa mmoja kati ya wahanga wa tukio la wikendi iliyopita ni kiongozi wa kijiji cha Monjane.

“Wanamlenga Chifu kwakuwa wanajua alikuwa akitoa taarifa kwa polisi kuhusu eneo ambalo al-Shabab wamejificha msituni,” alikaririwa.

Magaidi hao wanadaiwa kujipatia fedha nyingi kwa kufanya biashara ya mbao na ruby kwa kuteka sehemu ya maeneo hayo.

Kundi hilo la al-Shabab katika eneo la Msumbiji, lilianzishwa mwaka 2015 lakini halina uhusiano wa moja kwa moja unaofahamika kati yake na kundi la kigaidi la Al-Shabaab la nchini Somalia.

Urusi 2018: Nani atabeba Kombe? Tuimulike Iceland
Aliyeachiwa kwa muda gerezani afyatua risasi na kuua askari, raia

Comments

comments