Wananchi wenye hasira kali wamevamia kanisa katika eneo la Kanyogoga wilaya ya Gulu nchini Uganda na kuchoma kanisa moja muda mfupi baada ya ibada ya asubuhi, kwa madai kuwa linawaletea pepo wachafu.

Wakaazi wa eneo hilo lililoko Kaskazini mwa nchi hiyo wameeleza kuwa wamekuwa wakichukizwa na mienendo ya ibada ya kanisa hilo linalofahamika kama ‘Jesus is the Living Stone’ ambayo ni kinyume cha mafundisho ya Kikristo.

Mkaazi mmoja wa eneo hilo, Choowo Willy ameiambia New Vision ya Uganda kuwa kanisa hilo haliwaruhusu waumini wake kuoa au kuolewa. Aliongeza kuwa katika ibada za Jumapili waumini huingia wakiwa wamejifunika kama Waislamu na huacha viatu nje ya mlango.

Jeshi la polisi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa kanisa hilo lilikuwa limefungwa na Serikali lakini mchungaji wake alikaidi amri hiyo halali.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa eneo hilo, John Bosco Nyangkol ameeleza kuwa polisi walifika katika eneo la tukio na walimkamata mchungaji wa kanisa hilo kwa kukiuka amri halali ya Serikali.

Kaimu Kamanda Nyangkol alisema kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Video: Kakobe acharuka, Watoto 10 wachinjwa
Mgonjwa amuua mgonjwa mwenzake hospitalini, ajeruhi wauguzi