Wananchi wa kijiji cha Ndunyungu kilichopo Wilayani Liwale Mkoani Lindi wamelazimika kusimamisha msafara wa Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso alipokuwa njiani kwenda kukagua mradi wa maji wa Barikiwa Wilayani humo.

Wakiwa na mabango yaliyobeba ujumbe wa kumtaka Naibu Waziri awasaidie kupata maji, pia walieleza adha inayowakumba ya kusubiria maji kwa muda mrefu katika eneo wanalochotea maji, jambo ambalo linawasababishia kuchelewa kufanya shughuli za kimaendeleo.

Baada ya kuwasikiliza kero zao, Aweso alilazimika kwenda kuona chanzo pekee ambacho wananchi hao wanapata huduma ya maji, ambapo alijionea kisima kinachotumia pampu ya kusukuma kwa mkono na kuongea na wananchi waliojitokeza kwa wingi.

Amesema kuwa tayari mkandarasi anayejenga mradi kwa ajili ya kijiji hicho ameshalipwa pesa kiasi cha shilingi milioni mia moja na moja, hivyo hana sababu za kutokukamilisha mradi na kutokulipa vibarua waliochimba mitaro ya kufukia mabomba ya maji.

Aidha, akiwa katika kijiji cha Barikiwa suala la kutokulipwa kwa vibarua waliojenga mradi pia liliibuka jambo ambalo lilimlazimu kumsimamisha Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Liwale kujibu hoja za wananchi.

Hata hivyo, Aweso amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Liwale awasimamie wananchi hao walipwe kabla ya mwisho wa wiki ijayo. Naibu Waziri bado yupo Mkoani Lindi kwa ziara ya kikazi kwa kukagua miradi ya maji.

 

Lukaku kuitosa rasmi Man United? Mourinho ‘anakula bata’
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Desemba 8, 2018