Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka wananchi hususani wafugaji kutotumia matamko ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli vibaya kwa kutafuta mianya ya kutolipa kodi.

Ameyasema hayo akiwa katika mnada wa Upili wa Meserani uliopo wilaya ya Monduli Mkoani Arusha mara baada ya kufanya ziara ya kukagua utendaji kazi wa watumishi waliopo katika mnada huo na kusikiliza kero za wafugaji.

Amesema kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kipindi cha mwezi mmoja itashirikiana na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kutoa tafsiri sahihi ya mfanyabiashara mdogo anayestahili kukatiwa kitambulisho cha biashara ndogo ndogo (machinga) cha Shilingi Elfu Ishirini kwa mwaka.

“Mheshimiwa rais alikuwa amelenga hasa wale wafanyabiashara wadogo wadogo na tunachoamini tutaendelea kulifanyia kazi lakini suala la machinga kwamba naye mfanyabiashara wa ng’ombe kuhusishwa katika sifa za mfanyabiashara ndogondogo bado ni gumu kulitolea majibu, lakini ushauri tusitumie matamko ya rais vibaya tusitafute kichaka cha kujificha kwamba nawe ni machinga, wewe mwenyewe fikiria na jitafakari tulipe kodi na tujenge nchi yetu.” Amesema Prof. Gabriel

Aidha, Prof. Gabriel amepokea kilio cha wafugaji kuwa wamekuwa wakiuza ng’ombe kwa makadirio au matakwa ya mnunuzi kutokana na kutokuwepo kwa mizani ili waweze kuuza ng’ombe kwa kilo badala ya bei ya kukadiria kati ya mfugaji na mnunuzi wa ng’ombe, kitendo ambacho wafugaji hao wamesema kimekuwa kikiwafanya wasiuze mifugo yao kwa bei yenye tija kwao.

Pia amewataka wafugaji kufuga kisasa kwa kuhakikisha wanawapatia ng’ombe malisho bora ili wapate mazao bora ya mifugo yao huku Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikihakikisha inaendelea kuimarisha matibabu ili mifugo iwe na afya bora.

Kwa upande wake Kandidi Mlinyi ambaye ni msimamizi wa mnada wa Meserani amesema kuwa wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya upatikanaji wa maji katika ukanda wa Wilaya ya Monduli hivyo kuwa na mazingira magumu ya upatikanaji wa huduma hiyo mnadani.

 

 

Boomply yasaini mkataba na Warner Music
Habari Picha: JPM akutana na Naibu waziri mkuu wa Qatar