Wananchi wametakiwa kuacha tabia ya kuhifadhi fedha nyingi majumbani na badala yake wajenge utamaduni wa kuzipeleka benki kuepusha kuhatarisha usalama wao.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Desemba 5, 2016 wakati akifungua tawi la benki ya Biashara ya Uchumi lililopo wilayani Karatu mkoani Arusha akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani hapo.

Amesema tabia ya baadhi ya wananchi kuhifadhi kiasi kikubwa cha fedha majumbani si nzuri kwa sababu wanahatarisha usalama wao, hivyo ni vyema wakatumia benki mbalimbali zilizoko kwenye maeneo yao kwa ajili ya kutunza fedha zao.

Majaliwa amesema kufunguliwa kwa tawi hilo la benki kunaashiria ukuaji wa uchumi wa wilaya hiyo kwa kuwa benki ni kichocheo cha maendeleo.

Aidha, majaliwa ameushauri uongozi wa benki ya Uchumi kuangalia uwezekano wa kupunguza kiasi cha riba wanachokitoza katika mikopo wanayoitoa ili kuwawezesha wananchi kukopa na kupata tija.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo Bw. Wilson Ndesanjo alisema benki hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya mtaji mdogo jambo linalowasababisha washindwe kufungua matawi katika mikoa mingine.

“Changamoto nyingine ni baadhi ya wateja kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati, ambapo hatua za kisheria zikichukuliwa wanakimbilia mahakamani. Matukio haya yanadhoofisha kasi ya utoaji wa huduma kwani kesi zinachukua muda mrefu,” alisema.

 

Video: Hofu ya kutumbuliwa na JPM, Halmashauri zadaiwa kuficha taarifa za Kipindupindu
Msimamo wa Maalim Seif kuhusu mpango wa kuihama CUF wawekwa wazi