Jamii imeaswa kuacha unyanyasaji na ukatili kwa wakina Mama na Wasichana ili kuepusha vifo vitokanavyo na uzazi wakati wa kujifungua.

Wito huo umetolewa na Mratibu wa Muungano wa Utepe Mweupe Tanzania, Rose Mlay alipokuwa akizungumza na Dar24 Media baada ya semina waliyoitoa kwa watoa huduma ya jamii kutoka vituo mbalimbali vya kutolea huduma katika halmashauri ya wilaya Bukoba mkoani Kagera.

Amesema kuwa wanawake wamekuwa wakinyanyaswa pale wanapokuwa wakienda kujifungua, suala linalopelekea wengine kuchapwa na kufokewa na watoa huduma hali inayowafanya wakina Mama hao kujisikia wapweke kwa manyanyaso hayo.

Aidha, amesema kuwa watoa huduma ya jamii wanaowajibu wa kuielimisha jamii kuhusu ukatili na wao kujiepusha na vitendo hivyo ili kuwapa uhuru wanawake kujifungua kwa amani na kuwatunzia usiri kwa kuwatengenezea faragha wakati wa kujifungua.

“Wakina Mama na Wasichana wamekuwa wakipoteza maisha wakiwa wajawazito na wengine wakati wa kujifungua kutokana na kufanyiwa unyanyasaji, tunaiomba jamii kukemea sana vitendo hivi ili kujenga jamii inayojielewa na kupinga ukatili kwa akina mama na wasichana.”amesema Mlay

Kwa upande wao, watoa huduma ya jamii waliohudhuria semina hiyo wamesema kuwa wanashukuru kwa kupata fursa ya kuongezewa uelewa kwa baadhi ya mambo ambayo walikuwa hawayajui na kuahidi kueneza elimu ya kuzuia ukatili ili kujenga jamii yenye ustawi bora.

Muungano wa Utepe Mweupe Tanzania umekuwa ukielimisha jamii juu ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na wasichana ambapo kwa mkoa wa Kagera wanaendelea kutoa elimu hiyo katika wilaya za Bukoba na Muleba.

 

Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro yanufaika na Kilimo cha Umwagiliaji
TFDA yaja na mfumo mpya wa udhibiti usalama wa Chakula