Serikali ya Kenya imetoa saa 48 kwa watu wanaocheza michezo ya kubahatisha (betting) kuondoa fedha zao kwenye makampuni 27 yaliyoorodheshwa kufungiwa vinginevyo hawatazipata.

Tamko lililotolewa jana na Bodi ya Kudhibiti na Kutoa Leseni za Michezo ya Kubahatisha (BCLB) limeeleza kuwa akaunti za makampuni hayo zote zitafungwa baada ya muda huo na kwamba hakuna mtu atakayeruhusiwa tena kudai fedha zake.

“Ili kuwaruhusu wachezaji wa michezo ya kubahatisha kutoa fedha zao ambazo wanaweza kuwa wameziweka kwenye akaunti za makampuni haya yaliyoorodheshwa, tunatoa saa arobaini na nane kuanzia tarehe ya tangazo hili, na barua hii ni tamko rasmi lenye mamlaka,” linasomeka tamko lililosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Liti Wambua, Julai 11, 2019.

Wambua alieleza kuwa makampuni hayo 27 yalifungiwa kutokana na kukiuka sheria na kanuni za michezo ya kubahatisha.

Aidha, kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, akaunti za benki za makampuni hayo yaliyotajwa kufungiwa pia zitaathirika.

“Tumebaini kuwa benki za biashara zimetakiwa kufuata utaratibu ambao utasababisha makampuni hayo kushindwa kuchukua mabilioni ya fedha zao kuyahamishia nje ya nchi,” limeeleza gazeti hilo.

Aprili mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Fred Matiang’i aliagiza hadi kufikia Julai makampuni hayo yawe yamekamilisha taratibu za kukidhi matakwa ya sheria na kanuni za uendeshaji wa michezo ya kubahatisha.

Balozi Seif Iddi atoa neno kuhusu TANTRADE
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 12, 2019

Comments

comments