Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemwagiza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kufuatilia malipo yote ya Wagonjwa wanoenda kutibiwa nje ya nchi ili kubaini ubadhilifu unaofanywa na baadhi ya watu wasiowaaminifu.

Ametoa agizo hilo wakati akizindua miradi Saba ya huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Ziwa Bugando yenye thamani ya shilingi Bilion15, jambo litakalosaidia kurahisisha upatikanaji wa huduma bora kwa ukaribu pamoja na kuokoa kiasi cha fedha miongoni mwa wanaohitaji huduma.

Amesema kuwa kuna baadhi ya Watendaji waliona kupeleka Wagonjwa nje ya nchi kwaajili ya matibabu ni fursa yakujipatia kipato, jambo lililokuwa linapelekea hasara kubwa kwa nchi ya Tanzania kutokana na malipo kwa baadhi ya watu wasiostahili.

“Na kwasababu Waziri wa Afya yupo hapa, akafuatilie malipo yote ambayo tunatakiwa kulipa, kule nje , akikuta kuna malipo ya kulipa mtu ambaye hakuwa mgonjwa aliyejihifadhi huko, akazilipe mwenyewe,”amesema Rais Dkt. John Pombe Magufuli

Naye, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuwa hadi kufikia Juni 30, 2019 Serikali ina jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya vya umma 5756 (71%), Taasisi za Dini 923 (11%) na vituo vya watu binafsi ni 1440 (18%).

Waziri Ummy amesema kuwa Serikali, ina Jumla ya Vituo vya Afya vya Mashirika ya Dini ikiwemo Hospitali Teule za Wilaya vipatavyo 43, ambazo zinapata ruzuku (OC) kiasi cha shilingi 30,704,000/= kwa mwezi na mishahara kiasi cha Tshs.1.8 bilioni kwa mwezi kwa ajili ya watumishi 2600.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hospitali ya kanda ya Bugando Prof. Abel Makubi akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, amesema kuwa kwa kipindi cha miaka minne wamefanikiwa kuboresha huduma za afya na kukamilisha miradi saba ambayo ni  kitengo cha  saratani, mahututi, upasuaji, oksijeni na viwanda vidogo ambavyo vitakuwa vinazalisha dawa kwa ajili ya wagonjwa.

 

Zuma alia na hujuma, 'Wanampango wa kunipoteza kisiasa'
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 16, 2019