Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro amesema Serikali imezingatia suala la Haki za Binadamu kwa wakazi waliokuwa wanaishi Ngorongoro kisha kuamua kuanza kuondoka kwa hiyari yao kuelekea Kijiji Cha Msomera wilayani Handeni Mkoa wa Tanga.

Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo katika kikao na wadau wa Haki za Binadamu wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima.

“Serikali imezingatia vyema haki za binadamu, imewajengea nyumba wananchi walioamua kuhama kwa hiyari yao, imewapa maeneo yasiyopungua hekari 3 kila mmoja, imewasafirisha wao na mizigo yao na mifugo wanayomiliki, lakini pia Serikali imewalipa fidia”, ameeleza Dkt. Ndumbaro.

Waziri Ndumbaro amesema, imekuwa ni muhimu wadau wa Haki za Binadamu kukutana na kujadili suala la Ngorongoro na Loliondo ili kuhakikisha haki za binadamu zinazingatiwa na kujibu hoja zisizo za kweli zinazosambaa kwa haraka katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

Awali, Dkt. Ndumbaro alitoa wasilisho katika kikao na Mabalozi kutoka nchi mbalimbali na taasisi za kimataifa, liloonesha jinsi Serikali inavyozingatia haki na malengo yake kuboresha hali ya watanzania wa maeneo ya Ngorongoro na Loliondo.

Waziri Ndumbaro alisema kwa upande wa Loliondo, Serikali imewapa wananchi zaidi ya asilimia 62 ya eneo la hifadhi ya Loliondo ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa sasa na imebakiwa na kiasi cha Kilomita za mraba 1500 kutoka 4000 za awali.

Mawasilisho ya wataalam yameonesha umuhimu wa kuhifadhi maeneo ya Loliondo na Ngorongoro kutokana na sababu za kimazingira na Ikolojia.

TAMISEMI kuongeza uwezo huduma kwa wateja
Hassan Shehata amchana Mo Salah