Chama cha Wanasheria nchini Nigeria (NBA), kimewataka wanachama wake wote nchini humo kugoma kwenda mahakamani kwa lengo la kupinga hatua ya Rais Muhammadu Buhari kumsimamisha kazi Jaji Mkuu, Walter Onnoghen.

Kwa mujibu wa Reuters, NBA imewataka mawakili wote kutohudhuria kesi mahakamani kwa siku mbili ambazo ni Januari 29 na Januari 30. Uamuzi huo umechukuliwa baada ya Kamati Kuu ya Taifa ya NBA kukutana mapema leo.

Chama hicho cha wanasheria kinaungana na makundi mbalimbali pamoja na baadhi ya taasisi ambazo zimejitokeza hadharani kupinga hatua ya Rais Buhari kumsimamisha kazi Jaji Mkuu.

Buhari alichukua hatua hiyo dhidi ya Jaji Onnoghen Ijumaa iliyopita, kisha akamteua na kumuapisha Jaji Ibrahim Tanko Mohammed kuwa Kaimu Jaji Mkuu.

Alieleza kuwa uamuzi wake wa kumsimamisha kazi Jaji Mkuu ni kutekeleza mapendekezo ya Baraza la Maadili ya Utumishi wa Umma, ambalo lilieleza kuwa Jaji Mkuu hakutangaza mali na madeni yake kama inavyoelekezwa na sheria.

Uamuzi huo umekosolewa vikali na wapinzani wake, wakieleza kuwa unazua hali ya taharuki kwani zilikuwa zimebaki siku kadhaa Jaji Mkuu awaapishe wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Nigeria inatarajia kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu mwezi ujao.

Marekani na washirika wake wamekosoa vikali uamuzi huo, lakini Serikali ya Nigeria imejibu ikiitaka kutoingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Januari 29, 2019
Alvaro Morata aikacha Chelsea, aongeza nguvu Atletico Madrid