Serikali, imewataka Viongozi wa vyama vya siasa nchini, kuyatumia majukwaa ya kisiasa, kukemee biashara na matumizi ya dawa za kulevya, ikiwemo kutoa mafundisho yatakayowabadilisha wale wanaijihusisha na matumizi au uuzaji wa dawa hizo.

Wariri Mkuu, Kassim Majaliwa ameyasema hayo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya iliyoadhimishwa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar Es Salaam.

Amesema, wanasiasa hawana budi kutumia vikao na mikutano yao katika kupinga matumizi ya dawa za kulevya, sambamba na kuiunga mkono Serikali katika harakati zake za kutokomeza tatizo hilo nchini.

“Wanasiasa, tumieni vikao vyenu vya ngazi mbalimbali pamoja na mikutano ya hadhara kuunga mkono Serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, hili liende sambamba na majukwaa ya kisiasa mnapokuwa pale ielezeni jamii uhalisia,” amesisitiza Waziri Mkuu.

Kuhusu Viongozi wa dini kukemea suala hilo, Waziri Mkuu amewataka wanapotekeleza majukumu yao ya kiroho, wahakikishe pia wanakemea dhambi na uovu na kuweka msisitizo katika kukemea dawa za kulevya.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka watumie vyombo vyao vya habari kuendelea kukemea matumizi na biashara ya dawa za kulevya, ikiwemo kutoa habari kwa umma kuhusu huduma za waathirika wa dawa za kulevya zinazotolewa.

“Watangazieni Wananchi wote waweze kufahamu na kwa wale walioathirika waweze kutumia huduma zinazotolewa na hatimaye wapate tiba kamili na kuendelea kuchangia nguvu kazi ya taifa letu,” amesema.

Hata hivyo, ametumia fursa hiyo kuiasa jamii kuwalea watoto katika misingi ya maadili ili kuwaepusha na vitendo viovu ikiwemo matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya.

“Turejee kwenye asili yetu ambapo jamii nzima ilihusika katika malezi ya watoto na ilishirikiana katika kukemea maovu na ninawasihi wananchi tutambue wasafirishaji, wauzaji na watumiaji ni sehemu ya jamii, tuwe na uzalendo tutoe taarifa tukinyamaza tutazidi kuangamiza nguvu kazi,” amesisitiza Majaliwa.

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Gelard Kusaya amesema dawa za kulevya ni tatizo linaloathili maendeleo ya jamii hivyo wananchi wanatakiwa kushirikiana katika kudhibiti changamoto zinazotokana na matumizi ya dawa hizo.

Amesema, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambayo mwaka huu imetimiza miaka mitano tangu kuanzishwa kwake, huku ikifanikiwa kudhohofisha mitandao ya dawa za kulevya kwa kukamata wafanyabiashara na kuteketeza dawa hizo.

“Tumefanikiwa kudhibiti matumizi na athari zitokanazo na matumizi ya dawa za kulevya na nichukue nafasi hii kuvipongeza vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama kwa ushirikiano na kwa jitihada zao za kuhakikisha tatizo la dawa za kulevya linadhibitiwa,” amesema Kusaya.

Nao baadhi ya vijana waliokuwa wakitumia dawa za kulevya, wameishukuru Serikali kwa jitihada zake za kupambana na kuzuia matumizi ya dawa hizo nchini na kuwasihi vijana wenzao kutojiingiza katika matumizi hayo kwani madhara yake ni pamoja na kutoaminika, kutengwa na familia au jamii.

UN yalaani uvamizi majengo ya Bunge
RC aagizwa kuwashughulikiwa wafugaji wakorofi