Jumla ya wanaume milioni 4,456,511 wamefanyiwa tohara kinga ya kitabibu kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2009 hadi Septemba 2019 ilipoanza kutolewa nchini.

Afisa mipango kutoka mpango wa Taifa wa kudhibiti ukimwi (NACP), Dkt. Susan Mmbando ameyasema hayo wakati wa semina ya kuwajengea uelewa wabunge wa kamati ya Bunge ya masuala ya ukimwi, Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii pamoja na kamati ya Katiba na Sheria kuhusu mpango huo.

Amesema lengo la kwanza la hatua hiyo lilikuwa kuwafikia wanaume na vijana milioni 2.8 kufikia Septemba, 2017 ambapo hadi kufikia Septemba, 2017 waliweza kuwafikia wanaume milioni 3,303,940 na kuweza kuwatahiri.

“Katika lengo la pili kuanzia mwaka 2017 hadi 2022 tuna mpango wa kuwafikia wanaume milioni 2.7 na hadi kufikia Septemba, 2019 tayari tumeweza kuwatahiri jumla ya wanaume 1,681,070 ambao ni sawa na asilimia 60 ya lengo lililokusudiwa,” amebainisha Bi. Mmbando.

Aidha ameongeza kuwa hatua hiyo inatekelezwa katika mikoa 17 nchini yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) na kiwango kidogo cha utahiri nchini ambapo tayari Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto imeanza kutoa huduma ya tohara kwa watoto wachanga wenye umri kuanzia siku moja hadi 60 kuanzia mwaka 2013.

Amesema hatua hiyo ilifikiwa ili kuwa na huduma endelevu na kupunguza matatizo ya njia ya mkojo kama vile UTI uliotokana na utafiti wa kujifunzia yaani (pilot study), katika mkoa wa Iringa ambapo hadi sasa tayari wameifikia mikoa 15 nchini na kuongeza kuwa hadi kufikia Septemba, 2019 jumla ya watoto wachanga 13,603 wametahiriwa.

“Zoezi hili la tohara ya watoto wachanga linafanyika katika mikoa 15 nchini ambayo ni Iringa Njombe, Morogoro, Singida, Tabora, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita, Kagera, Rukwa, Katavi, Songwe, Mbeya na Kigoma kwa lengo la kupunguza matatizo ya njia ya mkojo,” amefafanua Bi. Mmbando.

Halima Mdee ajisalimisha Polisi, aswekwa rumande
Sababu kushamiri trakoma Singida zatajwa