Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka ametoa wito kwa Wanawake wenye tatizo la Ugonjwa wa Fistula kuacha kujificha na kujitokeza ili kwenda kupata matibabu ya ugonjwa huo yanayotolewa bila malipo.

Mhe. Mtaka ametoa wito huo Mei 3, 2022 katika uzinduzi wa kambi ya matibabu ya Fistula uliofanyika katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma (General).

Mkuu wa Mkoa Dodoma Antony Mtaka

“Nitoe wito kwa wanawake wote wanaosumbuliwa na tatizo la Fistula kutojificha kwa kuogopa aibu, wajitokeze na wafike katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ili wapate matibabu,” amesema Mtaka.

Mtaka amesema, Inakadiriwa kuwa, kwa mwaka wastani wa wanawake 2500 hadi 3000 hupatwa na ugonjwa wa Fistula wakati wa kujifungua, huku wanawake 30,000 ikisemekana kuwa na tatizo la Fistula nchini.

Aidha ameongeza kuwa Wizara ya Afya kupitia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari wa Fistula imeendelea kupambana dhidi ya ugonjwa wa Fistula kwa wanawake  hivyo kuwataka wanawake kujitokeza kupata matibabu yanayotolewa bila malipo huku huduma za nauli, chakula na malazi zikitolewa pia.

Aidha, Mtaka amebainisha athari kuu za ugonjwa huo zikiwa ni kupoteza uwezo wa kudhibiti haja ndogo au kubwa na kutokwa na haja ndogo na kubwa kwa wakati mmoja kupitia njia moja.

Mbali na hayo, Mtaka amewapongeza Wadau wote wa Fistula nchini kwa jitihada wanazoendelea kuzifanya kwa kushirikiana na Serikali katika mapambano ya kutokomeza ugonjwa wa Fistula nchini, huku akiwataka kuongeza kasi ya mapambano hayo ili kupunguza kiwango cha ugonjwa huo kabla ya mwaka 2030.

Wadau wa Fistula katika picha ya pamoja

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa tiba Wizara ya Afya Dkt. James Kihologwe amesema kuwa, Serikali imeongeza vituo vya afya vipya zaidi ya 480 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa wake wa kupambana dhidi ya ugonjwa wa Fistula hasa linalotokana na uzazi pingamizi.

“Serikali imeona tatizo la Fistula na hasa linalitokana na uzazi pingamizi, hivyo imeongeza vituo vya afya vipya zaidi ya 480 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa wake wa kupambana dhidi ya ugonjwa wa Fistula,” amesema.

Henock Inonga mchezaji BORA Simba SC
Jamii yaaswa kuwajali wenye ulemavu