Mamia ya wanawake katika vijiji vya Kirangi na Kuri, Kiambu nchini Kenya wameandamana Jumapili iliyopita wakipinga ongezeko la vilabu vya pombe (bars) na ulevi wa waume zao.

Wakizungumza wakati wa maandamano hayo ya amani, wanawake zaidi ya 100 wa eneo hilo walionesha hasira zao dhidi ya ulevi wa wanaume na watoto wao wa kiume.

“Unyanyasaji katika ndoa umeongezeka kutokana na matumizi ya pombe. Katika jengo hili la duka kubwa la manunuzi, tuna maduka manne pekee lakini bar ziko saba,” alilalamika mwanamke mmoja.

Ombi la wanawake hao kwa Rais Uhuru Kenyatta ni kuwachukulia hatua maafisa wa jeshi la polisi katika eneo hilo ambao wanadaiwa kupokea rushwa ili kulinda kumbi za starehe na bar katika eneo hilo tofauti na jitihada za Serikali kudhibiti ulevi hasa wa pombe haramu.

Walidai kuwa wanaume wao wamekuwa dhaifu wanaoshindwa kutimiza wajibu wao wa kifamilia akiongeza kuwa wengi wao wamekimbia nyumba zao. Waliongeza kuwa wengine walifikia hatua ya kuuza mali zao ili wapate pesa ya kununua pombe.

Maandamano hayo yamekuja wakati ambapo Serikali ya Kenya imeanza oparesheni ya kuharibu vifaa vya kutengeneza pombe haramu na kuwakamata wahusika.

Afrika kusini waandamana kushinikiza haki kifo cha Mtanzania aliyeuawa kikatili
Video: Moto wateketeza soko la Mbagala