Umoja wa wanawake wa kiislamu mkoani Kagera wawaomba wadau mbalimbali wa maendeleo kuwaunga mkono katika kumalizia ujenzi wa hospital ya mama na mtoto inayojengwa kata ya Nyanga Manispaa ya Bukoba.

Miongoni mwa masuala ya Kijamii yanayopewa kipaumbele kwa sasa ni pamoja na suala la Afya, ambapo kwa kutambua hilo Umoja wa Maendeleo ya Wanawake wa Kiislamu Kagera (UMWAKIKA) Kupitia Sadaka, michango yao na wahisani wengine walianzisha ujenzi wa hospitali ambayo kwa sasa ujenzi umefikia hatua mbalimbali.

Hajat Faidha Kainamula ni Mwenyekiti wa UWT – CCM Mkoa Kagera, akiwa Mgeni Rasmi katika Jaula na Harambee ya Uchangiaji wa Ujenzi  wa hospitali hiyo  amefurahishwa na jitihada za wanawake Hawa zenye lengo la kumkomboa Mwanamke juu ya huduma anayopatiwa.

Ameongeza kuwa Hospitali zimekuwa zikiwadhalilisha wanawake katika utoaji wa huduma, bila kujali Dini zao, lakini kukamilika kwa Hospitali ya Nyanga utakuwa mkombozi juu ya stara kwa wote bila kujali kabila wala dini zao.

“Niwaombe ndugu zangu waumini, wakina mama wenzangu na wananchi wote kwaujumla tujitolee kila tutakachojaaliwa ili tuweze kuukamilisha ujenzi huu, tumekuwa mashahidi juu ya mambo tunayokutana nayo katika hospitali zetu, ni maswahibu mengi yanatukumba na udhalilishaji mwingi hii ni kwasababu hatupati stara inayotakiwa kama wanawake” Amesema Hajat Faidha.

Katika Tamasha hilo jumla ya Shilingi Milioni Moja na laki tatu zimechangwa kupitia Michango yao na mnada wa mazao na vitu mbalimbali vilivyoletwa na wanawake wa Misikiti tofauti.

Ujenzi huo ulioanza miaka ya Nyuma, umekuwa ukisua sua kutokana na Nguvu yao kuwa kidogo, na Mara nyingi wamekuwa wakifanya matamasha na Harambee mbalimbali ili kusogeza mbele ujenzi.

Kufuatia hali hiyo umoja huo tayari umeanza maandalizi na mipango kwaajili ya Tamasha kubwa la Mwisho wa Mwaka litakalofanyika Desemba 27 hadi 29 Mwaka huu ambalo litawahusisha waumini kutoka maeneo mbalimbali.

Msekwa amuunga mkono Mkapa "wagombea wa upinzani walikuwa na hoja dhaifu"
Vyama vya msingi Kagera vyapata neema kutoka Benki ya TADB