Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza amewaonya vikali watu wote wanaokiuka amri iliyopitishwa na Serikali na kutaka hatua  kali kuchukuliwa kwa watu ambao wanaishi kwenye mahusiano kama mume na mke bila kufunga ndoa na kusajili ndoa zao.

Kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi Burundi, Serikali imeanza kuwachukulia hatua kwa  kukusanya ripoti za watu waliokiuka sheria hiyo iliyopitishwa na kutolewa mwaka jana ikiwataka watu wote kusajili ndoa zao kabla ya Disemba 31, 2017.

Nkurunziza ameitaka Serikali kuifuata sheria hiyo bila kujali sababu za kidini.

“Kwanza tunashukuru watu wote waliokuja kusajili ndoa zao serikalini kwa sasa watu ambao wamekaidi amri hiyo sheria itafuata mkondo wake, jambo lingine tumegundua tunajenga hoja za dini au madhehebu na kukaidi amri hiyo, dini haiwezi kuwa mpinzani wa sheria hatua hii itatusaidi kuzuia ongezeko la watu, maana yake leo hii ukiwa na wanawake watano utajikuta unakuwa na watoto 20 na sio tu wanakuwa hawatambuliwi kisheria lakini pia wanaleta shida nchini.“amesema Pierre Nkurunziza.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2017 kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Burundi, watu 166,000 wanaishi nje ya ndoa.

Hatua hiyo imepingwa vikali na wanaharakati nchini humo pamoja na waislamu  ambao hao kwa sheria za dini yao wanaruhusiwa kuoa mke zaidi ya mmoja ile hali amri ya serikali inakataza.

RC Wangabo apiga marufuku mwalo wa Kirando kutumika kama bandari
Mtuhumiwa bomba la mafuta ni mstaafu, Polisi watoa neno