Wabunge wa kambi ya upinzani wamesema watalihamishia sakata la utata wa Sh.1.5 Trilioni majimboni kwao baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhitimisha kuwa fedha hizo hazikuibiwa au kupotea.

Uamuzi huo wa wapinzani umetolewa na Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF). Bobali amesema kuwa ingawa kamati imehitimisha hivyo, wao wataendelea kuwasha moto akidai kuwa fedha hizo zilitumika bila idhini ya Bunge.

“Pale tunapohoji ni nani aliyeruhusu fedha hizo zikatumika bila idhini ya Bunge, na ni fedha nyingi. Sasa mjadala ndio kwanza unaanza na ni lazima moto uwake na ukweli ujulikane,” Mwananchi limemkariri Bobali.

Awali, Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa akisoma taarifa yake Bungeni alieleza kuwa uchunguzi wa kamati hiyo umebaini kuwa fedha hizo hazikuibiwa au kupotea kama ilivyokuwa ikidaiwa.

Alisema kuwa baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kupitiwa na kufanyiwa marekebisho, ilionekana kuwa suala la upotevu au wizi wa kiasi hicho cha fedha halipo.

Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai amewataka wananchi kuzingatia maelezo yaliyotolewa na PAC ambayo ni kamati inayoongozwa na wapinzani na kuachana na maelezo ya mtu mmoja mmoja ambayo amesema ni ya uongo.

Mwaka jana, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alidai kuwa ripoti ya CAG inaonesha kuna upotevu wa Sh.1.5 na kuitaka Serikali kulitolea ufafanuzi.

Siku chache baadaye, Rais John Magufuli akiwa Ikulu jijini Dar es Salaam, alimuuliza CAG kama kuna suala la wizi wa kiasi hicho cha fedha kwenye ripoti yake na msomi huyo wa mahesabu na fedha akasema hakuna.

Makamu wa Rais atoa neno baada ya kupata ajali ya ndege
Wasiochukua Vitambulisho Mtwara Watahadharishwa