Mabingwa wa Soka DR Congo TP Mazembe wameendelea kujiimarisha kuelekea Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Hatua ya Makundi inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa juma lijalo (Februari 12).
TP Mazembe imepangwa Kundi D sambmaba na Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, US Monastir (Tunisia) pamoja na Real Bamako (Mali).

Taarifa kutoka DR Congo zinaeleza kuwa, miamba hiyo ya Lubumbashi imekamilisha usajili wa Nahodha wa zamani wa Klabu ya Asante Kotoko SC ya Ghana Ismail Abdul-Ganiyu.

Beki huyo mwenye umri wa Miaka 26 amesaini Mkataba wa Miaka Miwili na Nusu, akitokea Asante Kotoko aliyoitumikia tangu mwaka 2019, akicheza michezo 69 na kufunga mabao sita.

Ganiyu anajiunga na wachezaji wengine waliosajiliwa TP Mazembe kupitia Dirisha Dogo la Usajili, ambao ni Mshambuliaji Michael Stephen (NIgeria), Beki wa Kulia Elie Madinda (DR Congo), Mshambuliaji Alex Ngonga (Zambia), Kiungo Mshambuliaji Gilroy Chimwemwe (Zimbabwe) na Mlinda Lango Narcisse Junior (Cameroon).

TP Mazembe itaanzia nyumbani Stade TP Mazembe, Lubumbashi kwa kuikabili Real Bamako (Mali) Februari 12, kisha itacheza dhidi ya Young Africans (Tanzania) jijini Dar es salaam katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Februari 19.

Mchezo watatu kwa Miamba hiyo ya DR Congo utachezwa Stade TP Mazembe, Lubumbashi dhidi ya US Monastir (Tunisia), Februari 26 huku timu hizo zikitarajia kurudiana mjini Tunis-Tunisia katika Dimba la Hammadi Agrebi, Machi 08.

Siku Kumi na moja baadae (Machi 19), Real Bamako (Mali) itaikaribisha TP Mazembe Stade du 26 Mars mjini Bamako, kabla ya timu hiyo kumalizia michezo yake Stade TP Mazembe, Lubumbashi kwa kuivaa Young Africans (Tanzania) Aprili 02.

Serikali yatoa siku saba uchafuzi wa mazingira kelele, mitetemo
Mdhamini mpya Simba SC kuidhinishwa CAF