Rais wa Zambia, Edgar Lungu ameonekana kuongoza kwa idadi chache ya kura katika matokeo ya awali yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zambia, (ECZ), huku upinzani ukidai kuwa hesabu zao zinaonesha mgombea wao ndiye anaeongoza.

Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo ulifanyika Agosti 11 mwaka huu, lakini hadi sasa matokeo kamili bado hayajatangazwa huku Katiba ya nchi hiyo ikiipa uhuru Tume ya Uchaguzi kutangaza matokeo rasmi ndani ya siku 7.

Lungu anakumbana na upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa chama cha United Party for National Development (UPND), Hakainde Hichilema ambaye alikuwa mkosoaji wake mkuu hususan kuhusu namna anavyotumia madini ya ‘Copper’ katika uchumi wa nchi hiyo inayoshika nafasi ya pili kwa kuzalisha madini hayo barani Afrika.

Katika tamko lao, UPND imedai kuwa tarakimu zao zimeonesha wazi kuwa Hichilema amemshinda Lungu katika asilimia 80 ya kura zilizohesabiwa, tamko lililopingwa na chama tawala kinachoamini pia kimeshinda.

Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi imevionya vyama vyote kutojihusisha na matamko yoyote yanayoeleza matokeo ya uchaguzi yasiyo rasmi, na kuiacha Tume hiyo kufanya kazi yake.

Kiongozi wa waangalizi wa uchaguzi huo kutoka nchi za jumuiya ya madola, Dkt. Jakaya Kikwete katika ripoti yake ameeleza kuwa uchaguzi ulifanyikwa kwa uhuru na haki na kuvitaka vyama vyote kuheshimu maamuzi ya wananchi.

Dkt. Kikwete alisema kuwa kulikuwa na dosari ndogondogo ambazo haziwezi kuathiri matokeo ya uchaguzi huo.

Pep Guardiola Kumuuza Joe Hart?
UVCCM waanza kutumbuana