Kocha Mkuu wa FC Platinum Norman Mapeza, amesema mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Simba SC, utakua na kila aina ya upinzani, kutokana na hitaji la timu hizo la kutaka kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Mapeza ambaye alikiongoza kikosi chake kuibuka na ushindi wa bao moja sifuri, amesema ameanza kuhisu mchezo wa jijini Dar es salaam kuwa mgumu kwao, kufuatia maandalizi na mipango iliyowekwa na wapinzani wao Simba SC.

Amesema jambo la kwanza ambalo linawapa ukakasi kuelekea mchezo huo ambao utachezwa Januari 06, 2021 ni kauli mbiu ya ‘WAR IN DAR’ (WIDA),  ambayo ilianza kupigiwa upatu saa chache baada ya mchezo wa mkondo wa kwanza kukamilika mjini Harare, Zimbabwe.

Jambo lingine lililozungumzwa na kocha huyo, ni ujasiri na umakini wa Simba SC wanapocheza kwenye uwanja wao wa nyumbani, huku akihofia kilichowahi kuwatokea Nkan FC, Al Ahly, JS Saoura na AS Vita.

“Ukweli uliowazi ni kwamba, wamekuwa na rekodi nzuri katika uwanja wao wa nyumbani, hilo jambo kiasi fulani linatia hofu lakini bado haiwezi kutukwamisha kusimamia mipango yetu, tumeshinda nyumbani lakini hata nje ya hapa bado tunahitaji matokeo bora.

 “Kuhusu kuwafuatulia wapinzani, kwetu linafanyika bila shida na ndiyo sababu kubwa inayotufanya kuanza maandalizi mapema.

”Simba imekuja na kauli mbiu hiyo ikiwa na maana kwamba vita ipo jijini Dar katika mchezo huo wa marudiano ambapo wachezaji wameahidi kucheza kwa uwezo wao wote ili kufuzu hatua ya makundi. Amesema Mapeza

Timu hizo zinatarajiwa kurudiana Januari 6, mwakani ambapo mshindi wa jumla atafuzu hatua ya makundi, huku atakayepoteza ataangukia hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba SC itatakiwa kushinda mabao mawili kwa sifuri na kuendelea ili kujihakikishia safari ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu, huku FC Platnum wakihitaji sare ama ushindi kufikia lengo la kuwatupa nje Mabingwa hao wa Tanzania Bara.

Manara: Nikiondoka, Simba nitamuachia nani?
Marekani yaripoti aina mpya ya virusi vya Corona