Waamuzi kutoka nchini Morocco wameteuliwa kuchezesha mechi ya ufunguzi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, kati ya wenyeji Mouloudia Olympique Bejaia na Yanga SC ya Tanzania Juni 19, mwaka huu.

Mchezo huo wa Kundi A utafanyika Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia, Algeria utachezeshwa na Bouchaib El Ahrach atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera, Redouane Achik na Youssef Mabrouk.

Baada ya mchezo huo, Yanga itarejea Dar es Salaam kuwakaribisha mabingwa wa Afrika, TP Mazembe Juni 28 katika mchezo wake wa pili wa Kundi A.

Na katika mchezo huo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limechanganya marefa kutoka nchi tatu tofauti, ambao ni Janny Sikazwe wa Zambia atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Jerson Emiliano Dos Santos wa Angola na Berhe O’michael wa Eritrea.

Timu nyingine katika Kundi A ni Medeama ya Ghana ambayo itafungua dimba na TP Mazembe mjini Lubumbashi Juni 17, mwaka huu, mchezo ambao utachezeshwa na marefa wa Shelisheli Bernard Camille, Hensley Danny Petrousse na Eldrick Adelaide.

Video: Magazeti Leo 09-Jun-2016
Mbeya City Wapiga Hatua Usajili Wa Kavumbagu