Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko amewataka waratibu wa dawati la Afya Moja kutekeleza dhana ya Afya Moja kwa wakati sambamba na kuweka mikakati mahususi itakayowaongoza katika utendaji wa dhana hiyo.

Ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha wadau wa afya moja na wataalam kutoka sekta ya Afya, Mifungo, Wanyamapori na Mazingira kilichofanyika Jijini Dodoma.

Amesema kuwa dhana ya afya moja inajumuisha wataalam na wadau mbalimbali kwa lengo la kufanikisha utekelezaji wa dhana hiyo ikiwemo kutoa fursa ya kushirikiana pamoja katika kukabiliana na madhara au magonjwa hatarishi nchini.

“Nimepitia Sera ya Afya moja na kuona suala hili linatakiwa kusimamiwa vyema, ikiwa Ofisi ya Waziri Mkuu ni mratibu wa Dawati la Afya moja kwa kushirikiana na Wizara, Taasisi za Serikali na wadau wa maendeleo, katika kuhakikisha nchi yetu inakuwa mahala salama,” amesema Mwaluko

Aidha, ameongeza kuwa, suala la kujenga uwezo kwa waratibu wa dawati la afya moja inatakiwa kuangalia ofisi kwa ujumla na si mjumbe mmoja tu ambaye atakuwa anasimamia masuala hayo ya Afya moja wakati wote.

“Mnatakiwa mtambue kuwa mkiwa kama wafanyakazi mna majukumu mengine ya kiofisi ambayo mnatakiwa kuyatekeleza, hivyo mtoe fursa kwa wafanyakazi wengine waliopo kwenye ofisi zenu kujifunza na kuelewa dhana hii ya afya moja,” ameongeza Mwaluko.

Kwa upande wake, Prof. Robinson Mdegela ambaye ni Mtaalamu Mshauri wa Afya Moja amesema kuwa kukutana kwao katika kikao hicho ni kuonyesha utayari wa kila mtaalamu katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuongeza msukumo juu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Afya Moja.

Utalii wa Sokwemtu kuanzishwa katika hifadhi ya Rumanyika
LIVE CHATO: Rais Magufuli akimpokea rais wa Uganda, Yoweri Museveni