Watu wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam kwa makosa ya kimtandao akiwemo Innocent Adam Chengula (23), aliyejipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia mtandao, akijinasibu kuwa yeye ni Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbas.

Mtuhumiwa huyo, amekuwa akiweka picha na majina ya Dkt. Hassan Abbas mtandaoni (Profile), na kutuma jumbe kwa watu akiwaomba wamtumie fedha kwenye namba tofauti za simu akiandika, “kaka naomba niazime 3mil alhamis nitakurudishia” au “kaka nina mtoto wangu naomba umpatie kazi apo kwako yeye amesomea bachelor of commerce in accounting.”

Katika tukio la pili, Jeshi la Polisi pia limemkamata Tazarn Alfan Mwambengo (27), mkazi wa Ukonga, ambae anatuhumiwa kusambaza taarifa za uongo kuhusu kifo cha Dkt. Harrison Mwakyembe kupitia Chaneli ya televisheni ya mtandaoni jambo ambalo si la kweli.

Kupitia Chanel hiyo, mtuhumiwa aliandika “BREAKING NEWS HUZUNI YATANDA MAZISHI YA MWAKYEMBE”. ambapo taarifa hizo, ziliibua taharuki kwa wananchi, Dkt. Mwakyembe mwenyewe na familia yake.

Watuhumiwa hao, wamekutwa na vifaa mbalimbali ambavyo wanavitumia kufanya uhalifu huo, ikiwemo Kompyuta mpakato (laptop) moja, Simu tatu, Maiki nne, Modem moja na Kadi za simu tisa za mitandao mbalimbali zenye usajili wa majina tofauti.

Aidha, Jeshi la Polisi linatoa rai kwa Watanzania kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii, pamoja na kuzingatia maadili ya taaluma ya Habari na sheria zinazohusika ili kuepuka kuchapisha taarifa zitakazo zua taharuki kwa umma, na kuwa makini wakati wa kutuma pesa au kufanya miamala kwa njia ya simu ili kuepuka kutapeliwa.

JTI yawapa Tabasamu wakulima zao la Tumbaku
Waandamana kudai fidia mabadiliko Tabianchi