Serikali nchini Uganda imeanzisha mfumo mpya wa kisheria ambapo washtakiwa katika kesi za adhabu kali kama vile mauaji watapewa fursa ya kujiamlia ni kiwango gani cha adhabu wapewe.

Katika mfumo huo mpya kuna matarajio kwamba mchakato wa kisheria wa kusikiliza kesi utakuwa wa haraka, utaokoa muda pamoja na gharama za kusikiliza kesi na kutoa hukumu.

katika mfumo huo mpya mshtakiwa ataweza kukiri kosa na kupewa muda wa kutoa adhabu dhidi yake hatua ambayo inatarajiwa kupunguza mrundikano wa kesi nchini Uganda kutokana na idadi ndogo ya majaji wa kusikiliza na kutoa hukumu kwa wakati mfupi na kwa haki.

Wakili na mwanasiasa Asuman Basalirwa ameiambia BBC kuwa mtuhumiwa atapewa fursa na jaji kukiri makosa aliyoyafanya na kumtaka jaji kumpatia kifungo hafifu.

“Mtu atakuwa na fursa ya kujadiliana kuhusu kiwango cha hukumu atakachopewa, iwapo mtu amefanya makosa atapelekwa mahakamani anapewa fursa na jaji kumwambia kwamba yeye alifanya makosa na anaomba kupewa hukumu ndogo” amesema wakili Basalirwa.

Takwimu za kitengo cha sheria katika jela kuu ya Luzira zinasema kuwa kuna takribani kesi 100 ni za adhabu ya kifo ama kifungo cha maisha.

Afisa mkuu wa mawasiliano katika kitengo cha sheria Solomon Muyita amesema kuwa katika sheria hiyo, makubaliano yatawasilishwa mbele, iwapo ni miaka 10 unaweza kuamua kwamba ingekuwa bora iwapo ungehudumia miaka miwili halafu mwendesha mashtaka anaweza kusema miaka miwili ni michache kwanini tusifanye mitano, unaweza kujadiliana kwa kutumia wakili ama hata wewe mwenyewe.

Miongoni mwa washtakiwa watakaonufaika chini ya mfumo huo ni wale wa kesi za mauaji, ubakaji, unajisi na ujambazi wa kutumia silaha.

 

 

 

 

 

 

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Juni 1, 2019
R Kelly akabiliwa na Mashtaka mapya 11