Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule leo Mei 29, 2023 ameendelea na ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mabweni katika Shule ya wasichana Bunge, ujenzi wa Shule mpya ya msingi katika eneo la Swaswa na madarasa ya awali katika Shule ya msingi Kisasa ambapo ujenzi wake uko katika hatua za ukamilishaji.

Katika kaguzi hizo, Senyamule ametoa maagizo kwa wasimamizi wa mradi kuhakikisha kazi inakamilika kwa muda uliopangwa na kuzingatia viwango vya ubora huku akitoa rai kwa wasimamizi wa ujenzi kukaa na mafundi ili kufanikisha ukamilishaji wake.

“Mkoa wa Dodoma tumejipanga kukamilisha hizi kazi kwa wakati hivyo wataalamu mkae na mafundi mpitie kwa pamoja mpango kazi wa miradi hii ili tujue kila siku ni kazi gani inatakiwa kukamilika kwa siku husika ili itakapofika tarehe 15 Juni 2023 ujenzi uwe umekamilika” amesisitiza.

Aidha, Senyamule amesema Serikali imetoa fedha zote kwa wakati hivyo hakuna sababu za kuchelewa kufanya manunuzi. Amesema ni wajibu wa wataalamu kuhakikisha ununuzi wa vifaa vyote vinavyohitajika vinapatikana ili mradi uweze kukamilika kwa muda uliopangwa.

Mkoa wa Dodoma, kupitia mradi wa Boost umepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 10.6 kwa ajili ujenzi wa Shule mpya 16, vyumba vya madasa ya msingi 163, madarasa ya awali 16, ujenzi wa vyoo 106, nyumba za walimu 3 na darasa 1 la elimu maalumu.

Shule ya Msingi Kisasa, imepokea kiasi cha Shilingi Milioni 63.6 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 2 na vyoo 6 huku Shule ya Swaswa imepokea kiasi cha Shilingi Milioni 318.8 kwa ajili ya kujenga Shule mpya itakayokuwa na madarasa ya msingi 7, madarasa ya awali 2 na Vyoo 12.

Aliyehukumiwa kimakosa aachiliwa huru baada ya miaka 33
Ripoti: Asilimia 10 ya watu Duniani wanalala na njaa