Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi, Kangi Lugola amesema hakuna Mtanzania yeyote ambaye namba yake ya simu itazuiwa kutumika kwasababu haijasajiliwa kwa kidole, kwa kigezo cha kutokuwa na kitambulisho cha Taifa.

Hivyo ikifika Desemba 31 mwaka huu, ambayo ilitajwa kuwa mwisho wa kusajili laini za simu kwa alama za vidole, kama mtu hajapata kitambulisho cha taifa laini yake ya simu haitazimwa na ataendela kuitumia.

Waziri Lugola ametoa agizo kwa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA), kuhakikisha kwamba maofisa wa NIDA wilaya zote wanapeleka namba za vitambulisho vijijini na si kutegemea kuzipata katika simu.

Aidha amewatoa hofu watanzania kuwa utaratibu wa utambuzi, usajili na utoaji wa vitambulisho kwa wananchi ambao wanasifa za kupata vitambulisho ni endelevu.

” Zoezi hili halina mwisho wala halina tarehe kwamba ikifika tarehe fulani kuna Mtanzania hajapata kitambulisho, basi huyo hatapata kitambulisho tena, Watanzania wasiwe na wasiwasi, hili ni zoezi endelevu na ndiyo maana kila mwaka kuna Watanzania ambao wanafikisha miaka 18″ amesema Lugola.

Amesema kuwa lengo usajili na utambuzi lilikuwa wananchi milioni 23.3, lakini hadi sasa wamesajili watanzania milioni 20.5na wamezalisha namba za vitambulisho kwa watanzania milioni 15.5.

Lugola alitoa maelekezo hayo jana bungeni, wakati akijibu mwongozo wa Mbunge wa kavuu, Dk Pudenciana Kikwembe (CCM), ambaye katika mwongozo wake alisema uandikishaji wa vitambulisho umekuwa na changamoto maeneo ya vijijini.

Idris amuomba msamaha Rais Magufuli, azungumzia kuhariri picha ya kitabu cha Mkapa
Mchakato wa kusaka tiketi AFCON 2021 waanza rasmi