Kufuatia matukio ya utekaji, kujeruhi na mauaji ya watoto wadogo yanayoendelea katika maeneo mbalimbali mkoani Njombe hatimaye madiwani wa Kata tofauti katika Halmashauri ya wilaya ya Njombe wameweka mikakati ya kukabiliana na janga hilo.

Wakizungumza na Dar24 Media Madiwani wa Kata za Mfriga, Kidegembye na Ikuna wamesema kuwa wameshtushwa na matukio hayo ya mauaji ya watoto wadogo yanayofanywa na watu wasiojulikana hivyo tayari wameamua kuunda mikakati maalumu ili kupambana na ujangili huo.

“Jambo hili tumelipokea kwa masikitiko makubwa sana hivyo kwasasa tumewatangazia wananchi wetu rasmi kuwa waanze kuwa makini na familia zao hasa watoto wadogo wanaosoma katika shule mbalimbali katika maeneo yetu pia watoe taarifa za uwepo wa wageni wasio na vibali vinavyowatambulisha wanakotoka,” wamesema madiwani hao.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Valentino Hongoli na Vasco Mbunda ambaye ni makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo kwa pamoja wamesema kuwa wametoa maelekezo kwa walimu wa shule zote za halmashuri hiyo kuwatangazia wanafunzi juu ya uwepo wa matukio hayo ikiwa pamoja na kuchukua hatua za kutembea pamoja katika makundi.

Aidha, wamesema kuwa mikakati mingine ni pamoja na kuwaagiza viongozi wa vijiji na kata kufanya mikutano ya mara kwa mara na wananchi wao kwa lengo la kupeana tahadhari pamoja na kuchukua hatua kwa watu ambao wanahisiwa kufanya vitendo vya ujambazi katika jamii.

Hata hivyo, wananchi mkoani Njombe wameitaka serikali kupitia jeshi la polisi kutoa tamkoa rasmi juu ya uwepo wa matukio hayo ya mauaji ya watoto ili kutokomeza kabisa pamoja na kuwakamata wahusika na kuwachukulia sheria.

Imani za kishirikina zatawala Njombe, wananchi walazwa chooni
Video: TPSF yawageukia wachimbaji wadogo wadogo wa madini

Comments

comments