Kutokana na kukithiri kwa tabia za waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda na abiria wao kutovaa helmet kichwani (kofia maalum ngumu) wakati wa safari, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameahidi kuwakamata na kuwafungulia mashtaka.

Akiongea katika hafla ya Futari iliyoandaliwa na Benki ya NMB kwa wateja na wadau jijini humo, Makonda alisema kuwa watu wanaotumia usafiri huo bila kuvaa helmet kichwani wanafanya kosa sawa na kutaka kujiua, hivyo watashtakiwa.

“Nimeshawasiliana na kamati yangu ya usalama barabarani mkoa, hili nitalisimamia kikamilifu lazima wote wawe na helmet na wakikamatwa wote watashtakiwa,” alisema Makonda.

Alifafanua kuwa kutovaa kofia hiyo maalum wakati umepanda usafiri huo, ni sawa na mtu anayetaka kujiua kwa kunywa vidonge na pombe kali.

Makonda alisisitiza kuwa atalisimamia kwa nguvu zoezi hilo hususan katika kipindi hiki cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ili aweze kupata dhawabu kwa Mungu kwa kuokoa maisha.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam alisema kuwa hivi karibuni atatangaza rasmi marufuku ya uvutaji wa sigara hadharani kwa sababu wanaofanya hivyo huwakera watu wasiovuta na huchangia kuchafua mazingira kwa kiasi kikubwa.

CCM yataja tarehe rasmi ya kumkabidhi Magufuli Uenyekiti
Belle 9 kuwapa zawadi nzito mashabiki wake, yuko tayari kushuka WCB